WAWILI MBARONI KWA MAKOSA YA UHUJUMU NA UHAMISHAJI HOLELA WA MITA ZA UMEME DAR ES SALAAM

Na Agnes Njaala, Dar es Salaam

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewafikisha mikononi mwa vyombo vya dola watuhumiwa wawili kutoka maeneo ya Madale kwa Kawawa na Tegeta kwa Ndevu baada ya kubainika wakijihusisha na makosa ya hujuma na uhamishaji holela wa mita kinyume na utaratibu.

Akizungumza Septemba 15, 2025 wakati wa operesheni maalumu ya ukaguzi, Afisa Usalama wa TANESCO, Lilian William, alisema taarifa zilipokelewa kupitia mfumo wa kupokea taarifa za siri wa TANESCO unaojulikana kwa jina ‘Whaistleblower’, zikihusu uharibifu wa miundombinu ya umeme katika moja ya nyumba iliyopo eneo la Madale kwa Kawawa, Dar es Salaam.

“ Mara baada ya kupata taarifa, tulifika eneo la tukio tulikuta nguzo ya umeme imekatwa na mita aina ya Bahdela imeng’olewa. Uchunguzi ulibaini aliyefanya kitendo hicho ni kibarua wa TANESCO anayeajiriwa kwa mkataba wa kikundi,” alifafanua Bi. Lilian .

Mtuhumiwa, Bw. Ally Salehe, alikiri kosa hilo na kueleza kuwa chanzo ni mgogoro wa kifamilia na mlezi wake, Bw. Imamu Salehe. Baada ya mahojiano zaidi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ilibainika kuwa pia alikuwa na vifaa vingine vya Shirika vilivyohifadhiwa kinyume cha utaratibu, ikiwemo mita moja (01) aina ya Inhemeter, Pg Clamp (100), Waya aina ya ABC wa 25mm wenye urefu wa mita 30, Viwasilianishi yaani ‘CIU’ (19) na Dion (05) vyote vikiwa mali ya TANESCO.

Mtuhumiwa huyo yupo mbaroni kwa hatua za kufunguliwa kesi ya uhujumu na baadae atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria kwani hata huduma hiyo aliyounganisha kwenye nyumba hiyo ya Baba yake mlezi ilikuwa ni kinyume na taratibu kutokana na usajili wa mita hiyo kusoma eneo la Mwananyamala.

Katika tukio jingine, ukaguzi uliofanyika eneo la Tegeta kwa Ndevu ulibaini mita tatu (03) zimehamishwa kinyume na utaratibu baada ya usajili wake kubainika kusoma maeneo tofauti na eneo ambalo mita hizo zimefungwa huku mpangaji wa eneo hilo la biashara Bw. Baraka Koyoyo akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi na hatua zaidi za kisheria.

TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa ‘Whistleblower’ katika kufichuchua matendo ya uhalifu yanayolihujumu Shirika kwani vitendo hivyo si tu vinaathiri mapato ya Shirika , bali pia vinarudisha nyuma maendeleo ya ustawi wa uchumi wa Taifa.

Shirika linasisitiza kuwa, litaendeleza ushirikiano na vyombo vya dola kuhakikisha wahalifu wanaothibitika kuwa na hatia wanachukuliwa hatua kali za kisheria ili kuzidi kuleta tija ya uwepo wa mfumo huo wa kimageuzi.