Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
SHULE ya Msingi ya Buguruni Viziwi imeibuka mshindi wa kwanza kitaifa katika mashindano ya ubunifu wa elimu ya usalama barabarani kwa mwaka 2025 (VIA Creative 2025), yanayoendeshwa na Kampuni ya Total Energies kwa kushirikiana na TotalEnergies Foundation pamoja na NafasiArt Space.
Washindi wa mashindano hayo ambayo yenye lengo la kuhamasisha utoaji wa elimu ya usalama barabarani kupitia ubunifu na sanaa kwa wanafunzi wametangazwa jijini Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo mbali na shule ya Msingi ya Buguruni Viziwi kushika nafasi ya kwanza,nafasi ya pili ilishikwa na shule ya Sekondari Ndalala iliyopo Temeke huku shule ya Msingi Ubungo NHC ikishika nafasi ya tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa kwa washindi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Tanzania, Mamadou Ngom, aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki katika mradi huo kwa ubunifu na dhamira yao ya kuimarisha usalama barabarani.

Alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya safari hiyo ya mabadiliko na kwamba kupitia elimu na uhamasishaji, wanachangia kujenga mustakabali salama kwa watoto na jamii ya kitanzania kwa ujumla.
“Idadi ya wanafunzi waliowezeshwa na VIA inaonyesha dhamira yetu ya dhati katika kulinda maisha na ustawi wa jamii zinazotuzunguka. Kujumuishwa kwa shule ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia ni hatua muhimu na ni ishara kwamba hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma,” aliongeza.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano TotalEnergies Getrude Mpangile alisema mradi huo ulizinduliwa Julai mwaka huu, katika Shule ya Sekondari Ndalala iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam na kwamba kwa kipindi cha miezi mitatu wanafunzi wameweza kujifunza na kupata uelewa juu ya mambo yote yanayohusu masuala ya usalama barabarani.
Amesema kutokana na matokeo waliyoyaona katika pindi cha miaka minne kupitia mradi huo, wataendelea kuutekeleza mwakani na miaka inayofuata, hivyo wanaendelea kuomba ushirikiano kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Elimu ili kuweza kuendelea kutekeleza mradi huo mashuleni,

“Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani wamekuwa ni wadau wetu wakubwa hivyo tunaomba tuendelee kushirikiana nao kwa sababu ni lengo letu kuhakikisha kwamba jamii ya kitanzania inakuwa salama wakiwemo watoto wetu ili waweze kufikia ndoto zao,” amesema
Aidha amesema shule iliyoibuka mshindi wa kwanza itaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kanda ya Afrika, na endapo watafanya vizuri, watakwenda hatua ya dunia itakayofanyika jijini Paris, Ufaransa.

Mpangile amebainisha kuwa tangu mwaka 2022, mradi huo umefikia zaidi ya watoto 50,000, na kuandaa mabalozi wa usalama barabarani 250 wanaotoa elimu mashuleni na katika jamii. Kwa mwaka huu pekee, zaidi ya watoto 10,000 wamefikiwa katika Dar es Salaam, ikilinganishwa na 6,000 mwaka jana, huku programu hiyo ikipanuliwa hadi Dodoma.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi amesema kuwa mradi huo umewasaidia wanafunzi wao kuongeza kujiamini na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wenzao. Aidha, amebainisha kuwa wanafunzi wamechangia kuboresha mazingira ya shule kwa kuweka tuta kwenye eneo lililokuwa likisababisha ajali.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Nafasi Art Space, Brighton Light, amesema kuwa programu hiyo inatumia mbinu ya mwanafunzi kumfundisha mwanafunzi kwa kutumia michoro, nyimbo, video na maigizo, jambo ambalo limeongeza hamasa na kueleweka kwa haraka kwa wanafunzi wanaoshiriki.
Wanafunzi walioshiriki pia wameeleza walichojifunza kupitia mradi huo.
Latifa Nassor, kutoka Shule ya Sekondari Ndala A, amesema kuwa wamepata uelewa mpana wa matumizi sahihi ya barabara, hususan njia za watembea kwa miguu.

Fadhili Bilali Adam, kutoka Shule ya Msingi Ubungo National Housing, amesema kuwa mradi umewasaidia kutambua athari za kutokuwepo kwa alama za usalama barabarani na ameiomba TotalEnergies kuyafanyia kazi maoni yao ili kuboresha usalama wa wanafunzi.


