MAMBO:DEMOKRASIA HAIDAIWI KWA VITOSHO

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

WATANZANIA  wameaswa kutofuata mikumbo na kufanya vurugu kwakigezo chakutafuta uhuru wa kisiasa kwakuwa demokra ya kweli haijengwi kwa mashinikizo, vitisho au siasa za misimamo mikali, bali hudaiwa kwakujenga hoja, ushindani wa sera na heshima kwa katiba na sheria za nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam l3o Desemba 23, 2025 aliyekuwa mgombea  Bavicha Taifa, Masoud Mambo alisema kila chama cha siasa kina haki ya kushiriki au kutoshiriki katika mchakato wowote wa kisiasa, lakini haki hiyo haiwezi na haitakiwi kutumika kama chombo cha kulazimisha nchi kuyumba au kuvuruga utulivu wa Taifa.

“Ni muhimu Watanzania watambue kwamba lengo la vyama vya siasa si kusambaratisha nchi, bali ni kushika dola ili kutekeleza sera zao kwa maendeleo ya nchi na wananchi wenyewe. Lengo hili haliwezi kufikiwa katika mazingira ya migawanyiko, machafuko, taharuki, chuki na uhasama wa kisiasa. Taifa lolote lisilo na amani, umoja na usalama, halina mustakabali wa maendeleo.

“Msisitizo mkubwa kwamba changamoto za kisiasa hazitatuliwi kwa maandamano na hamasa za uvunjifu wa amani, lugha za uchochezi, au kampeni za kuichafua nchi ndani na nje ya mipaka yake,”alisema Mambo.

Alisema  njia sahihi, ya kistaarabu na ya kizalendo ni kutumia meza ya mazungumzo na majadiliano ya wazi kwa hoja na ustahimilivu, mifumo ya kisheria iliyopo, na elimu ya uraia kwa wananchi kupitia kampeni zenye kujenga hoja ili wapime na kuamua kwa busara.

“Watanzania tukumbuke tukiruhusu siasa za kuvuruga amani zitawale, waathirika wa kwanza tutakuwa ni sisi wenyewe sio hao walio ughaibuni au wanasiasa wenye viza tayari kukimbilia ughaibuni. Maendeleo yatasimama, uchumi utadorora na ajira zitapotea hivyo gharama ya kuyajenga upya itabebwa na sisi wananchi wenyewe,”alisema Mambo.

Alisema kwa miongo mingi Tanzania imejenga heshima kubwa kimataifa kama nchi ya amani, umoja na utulivu wa kisiasa,sifa hii haikuja kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya umadhubuti wa serikali zetu, busara za viongozi wetu na uzalendo wa sisi wananchi wake. 

“Tanzania imekuwa kimbilio la watu waliokimbia machafuko ya kisiasa katika mataifa yao. Tusikubali historia hii tukufu ibatilishwe kwa matakwa ya kisiasa ya muda mfupi.

“Tuwakatae wanaohamasisha au kuunga mkono mikakati inayolenga kuingiza nchi kwenye machafuko, vurugu au migawanyiko ya kisiasa kwani hao ni wanapinga maslahi ya Taifa na ustawi wa wananchi. Bila amani, hakuna haki; bila utulivu, hakuna maendeleo; bila umoja wa kitaifa, hakuna Tanzania imara,”alisema Mambo.