SERIKALI KUANZISHA JUKWAA LA KIDIGITALI KUWAFIKIA VIJANA

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

WIZARA ya Vijana imejipanga kuhakikisha inawafikia vijana kwa urahisi   kwakuanzisha Jukwaa la Kidigitali la Huduma Jumuishi  (Youth Digital One Stop Platform) ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za ajira,mafunzo,fursa za mikopo,masoko na huduma nyingine.

Akizungumza jana Waziri wa Vijana Joel Nanauka alisema katika falsafa ya wizara  ya utoaji wa huduma, wamejipanga kuhakikisha Serikali inafikika kwa vijana kwa urahisi na kwa wakati, na tunatumia teknolojia kama nyenzo ya msingi ya kuharakisha huduma, kupokea maoni, na kuunganisha vijana na fursa. 

“Ndiyo maana tumeanza hatua za kuanzisha jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi (Youth Digital One Stop Platform) ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za ajira, mafunzo, fursa za mikopo, masoko, na huduma nyingine kwa namna iliyorahisishwa,”alise.a Nanauka.

Alisema katika ziara zao mikoani, tumebaini masuala muhimu yanayohitaji hatua za haraka ikiwemo uhitaji mkubwa wa ajira na mafunzo ya vitendo; changamoto ya taarifa duni kuhusu fursa zilizopo; upungufu wa mitaji na ushauri wa kibiashara,changamoto za masoko na uongezaji thamani.

“Pamoja na masuala ya maadili, afya ya akili, na matumizi ya dawa za kulevya. Taarifa ya kina ya uchambuzi wa masuala hayo imeandaliwa na Kitengo husika na itaendelea kutumika kuimarisha mipango yetu ya utekelezaji na uratibu wa wadau,”alisema Nanauka.

Alisema wameshafanya na wanaendelea kufanya kikao kazi na Maafisa Maendeleo ya Vijana wa Mikoa na Halmashauri (Mikoa 26 na Halmashauri 184) ili kuweka uelewa wa pamoja wa mwelekeo wa Wizara, kuimarisha uratibu wa utekelezaji, na kukubaliana mfumo wa ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa sahihi kuhusu vijana, programu, ajira na uwezeshaji katika maeneo yao.

Alisema katika kuimarisha ushiriki wa vijana, Serikali inaendelea kuimarisha majukwaa ya kuwakutanisha vijana ikiwemo VIJANA Platform, ambayo ni jukwaa la kusikiliza sauti za vijana, kujadili changamoto, na kuunganisha vijana na wadau. Jukwaa hili linaenda sambamba na hatua za kisheria na kiutendaji kuelekea ukamilishwaji wa mfumo wa ushiriki wa vijana kitaifa, ikiwemo taratibu za utekelezaji wa Baraza la Vijana.

“Katika eneo la ugunduzi na ubunifu, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kwa kuendeleza vituo atamizi na vituo vya kulea wabunifu (innovation hubs), pamoja na kuhamasisha ubunifu unaozalisha ajira na bidhaa/huduma zenye ushindani.

 Alisema tutaimarisha mifumo ya ulinzi wa kazi za ubunifu katika sanaa, michezo, filamu na muziki, ili vijana wanufaike kiuchumi kutokana na kazi zao.

Alisema.Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ina vituo vitatu vya maendeleo ya vijana, navyo ni Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro) na Marangu (Kilimanjaro). 

“Dhamira ya Serikali ni kuvifufua na kuviboresha ili viwe vituo hai vya kutoa ujuzi wa vitendo, kujenga nidhamu na uzalendo, na kuwezesha vijana kupata stadi za ujasiriamali na ajira. 

“Katika maboresho hayo, tunalenga pia kuwa na programu maalumu ya Open Coding School ili kuongeza ujuzi wa TEHAMA na uchumi wa kidijitali kwa vijana,utekelezaji wa ajenda hiyo unahitaji ushirikishwaji mpana wa wadau,”alisema Nanauka.

” Hivyo, Serikali itaendelea kujenga ushirikiano na sekta binafsi, mashirika ya kiraia, taasisi za fedha, vyuo na taasisi za utafiti, pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo, ili kuongeza rasilimali, ujuzi na ubunifu katika utekelezaji wa sera na programu za vijana, sambamba na kuepuka urudufu wa shughuli na kuongeza tija,”alisema Nanauka.