KAMISHNA MWENDA:MFUMO WA IDRAS UTASAIDIA KUSIMAMIA USAWA KATIKA ULIPAJI KODI

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni utaongeza wigo wa Kodi na kusimamia usawa katika ulipaji wa kodi.

Hayo yamebainishwa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alipokuwa akifungua mafunzo ya IDRAS kwa washauri wa kodi na wahasibu jijini Dar es Salaam, Januari 15, 2026 ambayo yatafanyika kwa siku tatu na kuendelea kwa makundi mengine kwa muda wiki mbili.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mfumo wa IDRAS unakwenda kufanya maboresho makubwa kwa mifumo ya kodi za ndani iliyopo na unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato kwa kuweka usawa katika makadirio ya kodi.

Amesema kupitia IDRAS wataweza kuwabaini na kuwabana wanaokwepa kodi kwa njia mbalimbali na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya huku wakiwezesha biashara za walipakodi na kuzilinda.

“Kuwezesha biashara za Walipakodi ni pamoja na kutunza kumbukumbuza zao, IDRAS itakapoanza kazi itakuwa muarobaini wa kutunza kumbukumbu za biashara za Walipakodi na zitakuwa salama” amesema Bw. Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema nia ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuona mifumo ya Taasisi za Serikali inasomana ili kuongeza uwazi na uwajibikaji na TRA inatekeleza kwa vitendo jambo hilo kupitia IDRAS ambayo itaiunganisha na taasisi nyingine za Serikali.

Amesema kupitia IDRAS walipakodi wataweza kutoa risiti za EFD bila kutumia mashine ambapo pia wataweza kupatiwa Hati/Cheti cha Uthibitisho wa kutokuwa na madeni ya Kodi (Tax Clearance) jambo ambalo linatarajiwa kurahisisha biashara.

“IDRAS itakapoanza itakuwa na manufaa makubwa kwa mlipakodi ambapo ataweza kufuatilia taarifa zake na maombi yoyote ambayo atakuwa amefanya TRA kupitia mfumo huo ambao ni muhimu sana hasa katika eneo la akaunti ya Mlipakodi” amesema Bw. Mwenda.

Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za ndani Bw. Alfred Mlegi amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa washauri wa kodi kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo uo ili kuongeza uelewa kwa jamii na walipakodi kuhusu mfumo huo.

Amesema mfumo huo una jumla ya Moduli 17 lakini 15 ndiyo zipo tayari kuanza kufanya kazi isipokuwa mbili za ukagudi na uchunguzi ambazo nazo zinaendelea kujengwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) CPA Victoria Soka amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao ya kushauri masuala ya kodi na kuwawezesha wateja wao kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa urahisi kupitia mfumo huo.

“IDRAS inakwenda kuturahisishia kazi ya usimamizi wa kodi kwa tunaowashauri kutokana na kuwa na taarifa zote za walipakodi ambazo zitawawezesha kupata huduma wakiwa mahala popote”