Na Mwandishi Wetu,Musoma
WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, tarehe 23 Februari, 2026 katika Ziara yake ya Kanda ya Ziwa ametembelea Bandari ya Musoma,na kusisitiza kuwa Serikali inakwenda kuikarabati ili kuendelea kufungua fursa za kiuchumi Mkoa wa Mara
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na ukarabati na maboresho ya bandari zote za maziwa Makuu zikiwemo za ziwa Nyasa, Tanganyika na ziwa Victoria kwa lengo la kuimarisha uchukuzi kwa njia ya maji nchini na kuongeza mapato ya wananchi na Mikoa husika sambamba na kufungua uchumi wa kikanda

Akizungumza baada ya kutembelea Bandari ya Musoma, Mkoani Mara Waziri mbarawa amesema Ziwa Victoria upande wa mkoa wa Mara ndiyo eneo pekee linalopakana na Nchi mbili za Uganda na Kenya hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kufanya maboresho ya bandari ya Musoma ili kuufungua Mkoa wa Mara na kuiufungua nchi Kikanda
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari, ujenzi na ukarabati wa Meli ili kuimarisha usafiri kwa njia ya maji katika Maziwa yote nchini kwa lengo la kuinganisha Tanzania na nchi jirani.

Akizungumza kwa niaba ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Alfredi Mtambi, amesema bandari ya Musoma ni bandari ya kimkakati, ambapo maboresho yake yataufanya mji wa Musoma kuwa kitovu kikubwa cha biashara, uvuvi na utalii kikanda
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Mhe. Mgore Miraji, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa majini nchini , akibainisha kuwa maboresho yatakayofanyika kwenye bandari ya Musoma, wananchi wake na wale wa maeneo ya jirani watanufaika moja kwa moja kupitia ongezeko la shughuli za kiuchumi na fursa za ajira.

Ziara hiyo ya Waziri wa Uchukuzi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kuboresha bandari za ndani ya maziwa makuu ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Maziwa yote makuu nchini.

