Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimefanya kikao cha pamoja cha wataalam wa sekta ya uchukuzi leo tarehe 18 Machi, 2026 Mkoani Kigoma, chenye lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya usafiri na kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho umeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara, huku ujumbe wa DRC ukiongozwa na Mratibu wa Shoroba za usafirishaji (CEPCOR) kutoka Wizara ya Uchukuzi, njia za Mawasiliano na Muunganiko, BW. Roger Te- Biasu.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Prof. Kahyarara amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa Meli mpya Nne, ukarabati wa MGR, reli ya TAZARA, Meli ya Mv Liemba ili kuendelea kuboresha muunganiko wa kikanda
Amesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na DRC kuhakikisha miradi iliyokubaliwa inatekelezwa kwa wakati, huku akibainisha kuwa Bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu za Kwala, Ihumwa, Isaka na hivi karibuni Morogoro zinaendelea kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya soko la kikanda.

Kwa upande wake, Roger Te- Biasu ameeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya uchukuzi, akisema hatua hizo zinafungua fursa kubwa kwa DRC kunufaika na huduma za usafirishaji wa Meli, bandari na reli.
Awali akitoa neno katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Ushoroba wa kati (CCTTFA), Adv. Okandju Flory ameeleza kuridhishwa na maboresho makubwa ya bandari zinazohudumia nchi za Ukanda wa Kati, hatua inayochochea ukuaji wa biashara baina ya nchi wanachama na kubainisha kuwa maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Kigoma yataongeza ufanisi wa usafiri wa anga Kimataifa na kufungua fursa zaidi za kiuchumi
Kikao hicho kilihitimishwa kwa kusainiwa kwa taarifa ya pamoja ya Kamati ya Uongozi na kwa kutembelea baadhi ya Miradi ya Uchukuzi hatua inayotarajiwa kuimarisha utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na kuongeza kasi ya maendeleo ya biashara kati ya Tanzania na DRC




