Ashrack Miraji Lushoto Tanga
Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Bagamoyo, Bi Ndimbumi Joram, akitoa elimu na ufafanuzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuhusu mradi wa uchimbaji mdogo wa madini ya bauxite ulioko kijiji cha Magamba, kata ya Magamba, wilaya ya Lushoto.
Halmashauri ya Lushoto iliomba kupata elimu ya kutosha ili kuwapa wananchi taarifa ya tathmini ya mazingira na jamii iliyofanywa hivi karibuni na kampuni ya Paulsam Geo Engineering Co Ltd na kufahamu faida za mradi huu.
Bi Ndimbumi alieleza kuwa mradi huu utaleta tija kubwa sana katika jamii na Halmashauri kupata mapato.
Aliwataka viongozi wasitumie siasa kwenye jambo hili la msingi lenye tija kubwa na maslahi mapana kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa elimu inayotolewa inapaswa kuwafikia wananchi ili waweze kuelewa mradi wa bauxite na siyo kuwapotosha.
Aidha, Bi Ndimbumi alifafanua kuwa serikali ndiyo inayoweka mifumo ya kufanya tathmini ya mazingira na kazi kubwa ya NEMC ni kusimamia na kukagua kampuni za tathmini za mazingira ambazo zimesajiliwa kisheria.
Alisema kuwa mwekezaji yeyote anayependa kumiliki mgodi mkubwa lazima afuate kanuni zilizopo kisheria.
“Naomba tusiwe na migogoro binafsi hasa kwenye swala la maendeleo ya Taifa letu,hili jambo ukiangalia kwa tasmini ya kawaida tu,udongo huu kwa asilimia kubwa unatumika kujengea barabara hapa wilayani,nyumba za wakazi wa huku na hakuna athari yoyote iliyojitokeza kwa wananchi”
Mhandisi wa Madini Mkoa wa Tanga, Laurent Bujashi, alikumbusha kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisisitiza kuwa hakuna shughuli za uchimbaji wa bauxite zitakazofanyika Magamba hadi tathmini ya mazingira itakapofanywa na wataalamu. Mradi huu ni mdogo ikilinganishwa na miradi mikubwa ya madini nchini.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lushoto na baadhi ya madiwani walionyesha kutoridhishwa na elimu iliyotolewa na Meneja wa NEMC Kanda ya Bagamoyo pamoja na kampuni ya Paulsam kuhusu tathmini ya mazingira ya mradi huo.