TADB yatoa gawio la kihistoria la Shilingi Bilioni 5.58 kwa Serikali


Faida yaongezeka kwa kasi ni asilimia 31% ya ukuaji kwa mwaka mmoja

Na Hubert Kiwale, DAR ES SALAAM

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza gawio la kihistoria la Shilingi bilioni 5.58 kwa Serikali ya Tanzania, ongezeko kubwa kutoka Shilingi milioni 850 mwaka uliopita. 

Hayo yamesemwa leo Aprili 17, 2025 jijini Dar es Salaam mara baada ya  Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanahisa uliofanyika leo na Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama,amepongeza mafanikio ya TADB kwa kusema:

“TADB ni taasisi ya kisera inayotoa mchango mkubwa kwenye mageuzi ya kilimo. Gawio hili linaonesha namna benki inavyoongeza thamani kwa uwekezaji wa Serikali, huku ikiboresha maisha ya Watanzania.”

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema mafanikio ya benki yanatokana na mikakati madhubuti ya upanuzi wa huduma:

“Faida yetu kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 31 hadi Shilingi bilioni 24.7 kutokana na kuongezeka kwa mikopo katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB,  Ishmael Kasekwa, amesisitiza wajibu wao wa kuhakikisha benki inabaki kwenye mstari wa mafanikio:

 “Bodi imejipanga kusimamia kwa weledi ili kuhakikisha TADB inatimiza dhamira ya kuleta mageuzi ya kweli kwenye kilimo cha Tanzania.”

Katika hatua inayoonyesha ufanisi wa mikakati ya benki, mikopo chechefu imeshuka kutoka 3.8% hadi 2.7%. Bw. Nyabundege ameongeza:

“Hili linaonesha siyo tu tunakopesha zaidi, bali pia tunahakikisha ubora wa mikopo na ufuatiliaji wa karibu.”

Thamani ya mali za TADB imepanda hadi Shilingi bilioni 917, na kitabu cha mikopo kimeongezeka hadi bilioni 534 ni ishara ya benki inayoimarika kimtaji na kiuendeshaji.

TADB imefungua Ofisi ya Kanda ya Magharibi mjini Tabora ili kuwahudumia wakulima wa Tabora, Katavi na Kigoma.

“Kupitia upanuzi huu, tunazidi kusogeza huduma karibu na wananchi wa maeneo ya vijijini,” alisema Bw. Nyabundege.

TADB ni benki ya kisera ya Serikali inayotoa huduma za kifedha nafuu na endelevu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kwa lengo la kuendeleza minyororo ya thamani na kukuza uchumi wa kilimo hapa nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya TADB,  Ishmael Kasekwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 17, 2025 baada ya kikao cha bodi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *