Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao kazi cha watendaji wa sekta ya sanaa,Utamaduni, na Michezo nchini kwa lengo la kujadili mipango ya utekelezaji wa sera,ilani,mikakati ya kitaifa na kimataifa katika ngazi ya Miji, Wilaya, Mikoa na Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Gerson Msigwa alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiandaa na kuratibu kikao kazi cha watendaji wa sekta za utamaduni, sanaa na michezo nchini ambapo kwa mwaka huu kinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.


“Kikao kazi cha mwaka 2025 ni cha 15 tangu kuanzishwa kwa vikao kazi hivi vya kimkakati mwaka 2003. Aidha,kikao kazi cha mwaka huu kitafanyika tarehe 22 – 25 Aprili, 2025 Katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
“Shabaha ya kikao kazi ni kujadili, kuibua, kuimarisha na kuendeleza fursa za kimkakati zilizopo katika Sekta za Utamaduni Sanaa na Michezo.
“Shabaha hii inatimia kwa kuendeleza ushirikiano baina ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na Mamlaka zilizoko chini yao katika utekelezaji wa majukumu,”alisema Msigwa.
Alisema washiriki wa kikao kazi cha mwaka huu ni pamoja na makatibu Tawala wa Mikoa,Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisa Utamaduni, Maafisa Maendeleo ya Michezo na Watendaji wote wa Sekta kutoka Taasisi za Kisekta na wadau.
Alisema shughuli zitakazofanyika katika kikao hicho ni pamoja na semina elekezi ya matumizi ya fursa za kiuchumi kwa jamii zitakazotokana na kuwapo kwa CHAN 2025 na AFCON 2027 nchini.
Alisema kwa kuwa wadau hawa ndio wasimamizi katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kikao kazi hicho ni fursa ya kuwajengea uwezo wa kuwaelimisha jamii na wadau kuchangamkia fursa za CHAN na AFCON zinazotarajiwa kujitokeza kwa wingi kutokana na maandalizi mazuri na mazingira bora kwa jamii kunufaika, yaliyowekwa bayana na Serikali.
“Semina elekezi ya kusimamia maadili ya Taifa katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,tunatambua kuwa dunia kwa sasa imekumbwa na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo kimsingi serikali inayahitaji katika maendeleo nchini lakini teknolojia hizi hazitakiwi kuja kuvunja misingi ya maadili yetu watanzania ambayo imejengwa kwa kipindi kirefu na mababu zetu,”alisema Msigwa.
Alisema semina hiyo elekezi inaenda kuwajengea uwezo Maafisa hao kuzingatia maadili ya mtanzania katika sekta ya utamaduni, sanaa na michezo na wapo manguli waliobobea katika ufahamu wa maadili ya nchi wakiongozwa na Profrsa Palamangamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Alisema kikao kazi hicho pia kitazindua mfumo wa usajili wa wadau wa Sanaa na utamaduni (AMIS) ambao unakwenda kuongeza ufanisi wa shughuli za Sanaa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema mfumo pia utawawezesha wadau na wasanii kuhudumiwa kwa haraka, kuibua vipaji vyao, kuhakikiwa kazi zao kwa haraka na kuondoa urasimu katika kazi za sanaa
Alisema kauli mbiu ya Kikao hiki ni Utamaduni, Sanaa, Michezo, Msingi wa Maadili ya Mtanzania; Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.