WANANCHI WA  MAGAMBA WATOA WITO KWA SERIKALI KUHUSU VIBALI VYA MGODI WA BOXIATE 

Na Ashrack Miraji  Lushoto Tanga

Tanga: Wananchi wa Kata ya Magamba, wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wameiomba Serikali kutoa vibali kwa wawekezaji wa mgodi wa boxite ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magamba, Mahamudu Kikoti, alizungumza na mwandishi wetu na kusema kuwa mradi huu ni fursa kubwa kwa vijana wengi kijijini kupata ajira na kujikwamua kiuchumi, pamoja na Halmashauri yao kupata kipato.

“Kwa niaba ya wananchi, mimi mwenyekiti wao, tumesubiri kwa muda mrefu sana mradi huu wa boxite uanze. Natumia fursa hii kuiomba Serikali kutoa kibali kwa mwekezaji ili aweze kuanza uchimbaji wa udongo wa boxite. Hii italeta tija kubwa sana kwa wananchi, hasa katika kupata huduma bora za kijamii kama zahanati, barabara, na maji, ambazo zimekuwa changamoto kubwa kijijini kwetu,” alisema Kikoti.

Kikoti aliongeza kuwa Halmashauri ya Bumbuli inachimba na wananchi wananufaika sana na mradi huo kwa kujipatia kipato na kujikwamua kwenye maisha.

 “Tunaona Bumbuli inakusanya mapato makubwa kuliko Lushoto kwa sababu wawekezaji wa Lushoto wanapata changamoto kubwa kwa kucheleweshewa vibali,” alieleza.

Mwenyekiti huyo alimalizia kwa kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anafahamika kwa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla, kuona vijana wanajikwamua kimaisha na kusaidia familia zao na kulijenga taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *