Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAZIRI Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amezindua huduma maalum ya kutoa taarifa kuhusu utapeli kupitia Akili Mnemba (AI) ambayo imetengenezwa mahususi kwa ajili ya kuwatahadharisha wateja dhidi ya ulaghai na utapeli wa kwa njia ya simu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es salaam Waziri aliipongeza Airtel kwa kutengeneza teknolojia ya kibunifu ambayo inaunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na matukio ya utapeli wa mtandao.
Alisema Huduma hiyo itamuwezesha kila mtumiaji wa simu janja na simu ya kawaida kuweza kunufaika nayo bila kulipia garama yoyote ile kwa kutumia Teknlojia ya akili mnemba airtel itaweza kutambua ujumbe za kitapeli na kutaoa tahadhari kwa watumiaji hapo hapo na kuwakataa matapeli.

“Matukio ya udanganyifu kupitia ujumbe wa massage yamekuwa yakiongezeka kwa kasi ambapo watu wamekuwa wakipokea ujumbe kutoka kwa namba ambazo wananchi hawazijui zinadai kutoa huduma au ofa kwa mitando au taasisi za serikali lengo likiwa ni kujipatia taarifa binafsi kwa lengo lakutenda uhalifu wa kimtandao” amesema waziri.
Ameongeza kuwa Huduma hiyo ya Airtel Spam Alert Kataa Matapeli inayotumia itaenda kuungamkono jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na wanaweza kuepukana na utapeli wa kimtandao kwa haraka zaidi.
Aidha ametoa rai kwa wadau wengine kuja na njia mbadala za matumizi ya teknlojia mbalimbali ikiwemo teknlojia ya akili mnemba kwajili ya kuhakikisha watumiaji ws huduma za kimtandao hawatapeliki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema kuwa suluhisho hili la kisasa la AI ni uthibitisho wa dhamira ya Airtel kuwawezesha wateja wake dhidi ya vitisho vinavyotokana na matapeli wa simu za mkononi, na kwamba huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli inapatikana kwa watumiaji wote wa simu janja na simu za kawaida.
“Huduma ya Airtel Spam Alert-Kataa Matapeli tayari inapatikana kwa wateja wote wanaotumia simu janja au simu ya kawaida, na muhimu zaidi, wateja wetu hawatahitajika kupakua programu yoyote au kufuata hatua za kuiwasha. Hii si tu tangazo la teknolojia kuhusu hatua muhimu ya kulinda wateja, bali ni tamko kwamba Airtel Tanzania si mtandao wako tu, bali pia ni mlezi wako wa kidijitali. Tumejitoa kikamilifu kuwawezesha wateja wetu kuwa makini na kuwapa imani ya kufurahia manufaa ya mawasiliano ya kidijitali,” amesema
Kamoto pia alitoa wito kwa wadau wa sekta ya mawasiliano kuunga mkono juhudi zinazolenga kukabiliana na udanganyifu wa simu katika jamii