Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekamata mtu mmoja aliyekuwa akitoa huduma ya kutengeneza vitambulishi vya Taifa katika eneo la Chalinze kinyume na sheria.
Akizungumza leo Mei 2, 2024, Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA, Geofrey Tengeneza amesema mtuhumiwa huyo aitwaye Danford Mathias mkazi wa Chalinze mkoani Pwani alikamatwa Aprili 23, 2025 saa 9 alasiri baada yakuwekewa mtego kwa kosa la kujihusisha na utengenezaji na uchapishaji wa vitambulisho vya Taifa bandia.
Amesema mtuhmiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hivi karibuni atafikishwa mahakamani kwa hatua zingine za kisheria.

Tengeneza amesema walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyu baada ya kupata taarifa zake za kujihusisha na vitendo hivyo vya utengenezaji wa vitambulisho bandia, NIDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata pamoja na vifaa vyake baada ya kutengeneza kitambulisho kwa malipo ya Sh. 10,000.
“Mtuhumiwa huyu alikuwa akitengenezea wateja vitambulisho feki katika steshenari yake iliyopo Msata Chalinze kwa malipo kati ya Sh. 6000 hadi 10,000, Katika kutengeneza na kuchapisha vutambulisho feki, Mathias hutumia kitambulisho chake halali cha NIDA na kuki-scan kisha kukiingiza kwenye mfumo wa Adobe na kufuta taarifa zake.
“Akifuta taarifa zake anabandika taarifa za mteja ikiwemo namba ya utambulisho wa Taifa -NIN, picha, majina, saini na kuwawekea tarehe zinazoonyesha ukomo wa matumizi ya kitambulisho hicho yaani expiry date, zilizo kwenye kitambulisho chake huyo mtuhumiwa kabla ya kuprint kitambulisho bandia na kumkabidhi mteja,” amesema Tengeneza
Hata hivyo Tengeneza amewataka wamiliki wote wa maduka ya steshenari kutojihusisha kwa namna yeyote ile na utengenezaji au uchapishaji wa vitambulisho feki vya Taifa kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na ni kinyume cha sheria ya usajili na utambuzi sura ya 36 ya mwaka 2012, kanuni ya usajili na utambuzi wa watu ya mwaka 2014 na sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 mwaka 2022.
“Nitoe wito kwa wananchi wenye namba za utambulisho wa Taifa kuwa wavumilivu wanapopewa muda wa siku chache kusubiri vitambulisho vyao kuzalishwa kwani kwa sasa huchukua majuma mawili mpaka matatu tu kuzalishwa baada ya kukamilisha usajili,” amesema