KIHENZILE AWATAKA WATALAAM WA LOGISTIKI KUWASAIDIA MADEREVA KUPATA STAHIKI ZAO

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amezindua rasmi Chama cha Wataalam wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA) huku alisisitiza kuangalia maslahi ya madereva likiwemo maslahi ili kuwasaidia wanapopata changamoto kazini.

Alisema ni muda sahihi sasa wa chama kukaa chini kuangalia na kupata majibu ya changamoto zilizopo na kuzifanyia maboresho.

“Chama kikae chini kiangalie majibu ya changamoto kuu zilizopo ,tazameni maboresho mbalimbali naombeni muwasimamie kuhakikisha madereva wa sekta binafsi na serikali kuhakikisha wanapata maslahi yao,”alisema Kihenzile.

Alisema ni muhimu mtumishi kupata maslahi yake kwakuwa inamsaidia kupambana na changamoto anapopata matatizo kazini.

“Kuna baadhi ya watu hawapelekei angalia kama kuna mtu kama katoa ushuhuda kwamba alipata matatizo lakini alivyopata stahiki zake zilimsaidia,fikiria ungekuwa wewe umepata matatizo alafu usipate stahiki zako ungejisikiaje,”alisema Kihenzile.

Alisisitiza kuwa chama hicho ni mhimili muhimu katika kuimarisha weledi na utoaji wa huduma bora katika sekta ya uchukuzi nchini.

Akizungumza jana kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa katika hafla ya uzinduzi huo,Kihenzile alisema TALTA inawakilisha wataalam wenye elimu na uzoefu wa ngazi mbalimbali na itakuwa kichocheo katika kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Wataalam wa Uchukuzi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya uchukuzi kupitia reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na vyuo vya mafunzo ili kukuza usafirishaji nchini na vyote hivi vinahitaji wataalamu wa kuvihudumia na kuvitunza

Alisisitiza kuwa TALTA itakuwa na jukumu la kulinda maslahi ya wataalam, kutoa ushauri kwa sekta ya umma na binafsi, kuandaa tafiti na mafunzo na kuwa kiungo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia sekta ya uchukuzi.

Alitoa rai kwa wataalam wote wa sekta ya Uchukuzi kujiunga na TALTA, Taaasisi za Serikali na binafsi kuwapa fursa wataalam wao kujiunga, na uongozi wa TALTA kuhakikisha chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata katiba, weledi na kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.

Akitoa Salam za Wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Usafiri Andrew Magombana ameahidi ushirikiano wa karibu na TALTA katika kutekeleza Sera,Mikakati na maboresho ya huduma za uchukuzi kwa lengobla kuhakikisha usalama,ufanisi na haki kwa watumiaji wote

Kwa upande wake rais wa TALTA Alphonce Mwingira ameeleza dhamira ya chama ni kuwaunganisha wataalam kwa njia mbalimbali na kushirikiana na Serikali na sekta binafsi katika kukuza taaluma ya lojistiki na usafirishaji huku akisisitiza kigezo cha kuwa mwanachama ni kuwa na elimu ya ngazi yoyote ya lojistiki na usafirishaji kutoka chuo kinachotambulika na Serikali.

Katika Uzinduzi huo uliohudhuriwa na washiriki kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, vyama vya usafirishaji, madereva, wamiliki wa magari ya abiria, na wanafunzi wa Vyuo, Tuzo mbalimbali zilitolewa kwa Viongozi Wakuu wa Nchi, Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi katika kuutambua mchango wao kwenye sekta ya lojistiki na usafirishaji nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *