Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejenti ya Utumishi na Utawala Bora George Simbachawene Tanzania na Afrika inahitaji viongozi wa kimageuzi ili kuhamasisha juhudi za pamoja kuelekea kutimiza malengo ya maendeleo jumuishi na endelevu ya barani humo.
Simbachawene alitoa kauli hiyo Leo Mei 16, 2025 wakati wa mahafali ya nane ya programu za uongozi zinatolewa na Taasisi ya Uongozi ambapo jumla wahitimu 210 walipata vyeti katika ngazi mbalimbali.

Alisema watu wote watambue kuwa, viongozi wa kimageuzi wana sifa ya kuwa na maono ya kuleta mabadiliko,wana uwezo wa kufanya maamuzi ya kimkakati, kuibua fursa mpya za Maendeleo, kuwasilisha na kushawishi mipango ya muda mfupi na mrefu ya kukuza uchumi na kuboresha hali ya maisha ya jamii zetu.
“Hivyo, Tanzania na Afrika kwa ujumla inahitaji viongozi wa kimageuzi katika kuhamasisha juhudi za pamoja kuelekea kutimiza malengo ya pamoja kwa kuhamasisha uvumbuzi, kuongoza mabadiliko katika nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuandaa na kutekeleza Sera zinazokuza maendeleo jumuishi na endelevu ya Bara letu la Afrika,”alisema Simbachawene.

Alisema ninatumaini mafunzo mliyoyapata yatawasaidia kuwa na maono, kusimamia utekelezaji wa mipango yetu pamoja na kupima na kufanya mapitio ya matokeo ya utekelezaji wake. Aidha, ni matumaini yangu pia mtakuwa na uwezo mkubwa wa kutambua fursa na kuchangia katika kuweka mazingira mazuri ya kiuongozi yatakayochochea kuleta maendeleo endelevu nchini mwenu.
“Mafunzo mliyoyapata yawafanye kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo yenu ya kazi, na tunaamini mtakwenda kukuza na kuimarisha utawala bora kwa kufuata haki, sheria, kanuni, miongozo na taratibu tulizojiwekea, kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ubunifu na kuimarisha utendaji wa kazi ili kulisaidia taifa kufikia malengo tuliyojiwekea,”alisema Simbachawene.

Alisema ili kufikia malengo makuu ya kuleta maendeleo endelevu Afrika, amewasihi tasisi ya Uongozi kuongeza kasi ya kupanua wigo wa Programu zake ili ziwafikie viongozi wengi zaidi wa Afrika.
“Katika kuhakikisha programu hizi zinakuwa jumuishi na endelevu Barani Afrika mfumo bora na rafiki wa kuchangia gharama uandaliwe.
” Ninatambua kuwa mmeshaanza kufanya hivyo na leo tuna wahitimu kutoka nchi nyingine za Afrika. Ninashauri tuongeze jitihada hizi ili kukuza uongozi wa mabadiliko na kuchangia Juhudi za mapinduzi ya kiuchumi barani Afrika.

Alisema suala la uratibu wa shughuli za Serikali, pamoja na uratibu wa miradi ya maendeleo umekuwa na changamoto nyingi zinazoathiri ufanisi.
“Hili nililisema mwaka jana katika mahafali ya saba. Naomba leo nirudie tena kutoa rai kwenu, huko muendako mkasaidie kutafuta namna bora zaidi za kuratibu utekelezaji wa miradi katika njia itakayosaidia matumizi ya rasimali fedha na watu ili ilete matokeo makubwa na chanya.
“Kama mnavyofahamu, Serikali inawekeza pesa nyingi sana katika miradi hiyo ili kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi,”alisema Simbachawene.

Alisema jambo hili litawezekana kama tutaimarisha mawasiliano na mahusiano na wadau wetu wa masuala ya maendeleo ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
Alisema Uongozi bora ni nguzo ya Maendeleo Endelevu ya nchi hivyo basi, ni jukumu la watu sote kama Taifa kuhakikisha tunakuwa na viongozi bora wenye sifa na uwezo wa kuongoza kimkakati.
‘Hili litafanikiwa kwa kuwa na mikakati thabiti ya kuwajenga na kuwaendeleza viongozi,mikakati hii ni pamoja na kuwa na programu maalumu za kuendeleza viongozi wa ngazi za juu na wanaochipukia katika sekta ya umma na bila kuacha nyuma sekta binafsi na asasi zisizo za Kiserikali.
” Ninafahamu Taasisi ya Uongozi imeanza maandalizi ya kuwa na programu maalumu ya kuwezesha viongozi chipukizi (emerging leaders programme). Viongozi hawa ni muhimu sana kwani wana kipindi kirefu cha kutumikia taifa letu wakati wa sasa na baadaye,”alisema Simbachawene.
Alisema programu hizo za kuwandaa na kuwajenga mapema kutaisaidia Serikali kuwa na kundi la Viongozi ambao wanaweza kupatikana pale watakapohitajika kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi,”alisema Simbachawene.
Naye mke wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb, amewashauri viongozi nchini kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, utawala bora na kufanya maamuzi mbalimbali kwa kuzingatia ukweli.
Alisema kuwa kuna madhara ya taarifa potofu na upotoshaji kwa sasa kutokana na maendeleo ya teknolojia ni makubwa, hivyo viongozi wanapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli na si kwa dhana au hisia.

“Tukizungumzia siku za usoni, maamuzi yetu yatazingatia yale ambayo mmefundishwa katika mafunzo yetu, niendelee kuwashauri kuwa mnapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli bila kuwaumiza wananchi,” amesema Innes-Stubb
Aidha mke huyo wa Rais wa Finland amesisitiza kuwa ni muhimu na lazima viongozi nchini kuhakikisha hawafanyi maamuzi yatakayowaumiza wananchi bali kufanya mambo kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.
