TTB YATEULIWA KUANDAA TUZO ZA UTALII UKANDA WA AFRIKA

Na Aziza Masoud,Dar es salaam.

ZAIDI ya washiriki 500 kutoka nchi mbalimbali duniani ambao ni wadau wa utalii wanatarajiwa kushiriki tuzo za 32 za kimataifa utalii wa Ukanda wa Afrika na Bara la Hindi zinazotarajiwa kufanyika nchini Juni 26 mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini (TTB) Balozi Ephraim Mafuru alisema lengo la Tuzo hizo ni kutambua mchango wa wadau wa sekta ya  utalii Duniani waliopo katika nyanja mbalimbali.

Alisema katika shughuli hiyo ambayo Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji  tuzo za utalii zitatolewa katika nyanja mbalimbali.

“Uwepo wa tuzo hizi nchini ni jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amekubali kutoa fursa katika sekta ya utalii, tunapaswa tumpongeze Tuzo kama hizi ziliwahi kufanyika miaka ya nyuma ambapo hazikuwa kwa ukubwa kama ilivyo sasa”,alisema Mafuru.

Alisema kuchaguliwa kwa Tanzania kuwe mwenyeji wa Tuzo hizo kwa nchi za Afrika pia kumetokana na ushindi wanchi katika tuzo zilizopita kwani iliongoza kwa kuwa na tuzo 5 tofauti na nchi nyingine za Afrika.

“Shughuli kama hii mwaka jana 2024 ilifanyika Mombasa kenya Tanzania ili shinda tuzo tano ambapo bodi bora ya utalii ya utalii Afrika ilichukua TTB,kivutio bora cha utalii Afrika ilikuwa mlima Kilimanjaro, hifadhi ya taifa bora Afrika ilikuwa Serengeti, kivutio bora cha safari Duniani sasa mafanikio haya hayaji tu hivi hivi ni kazi kubwa imefanyika ikiongozwa na Rais wetu”,Amesema.

Alisema katika tuzo hizo Kwa Tanzania  kampuni 50 zinazojihusisha na utalii zitashiriki ambapo washiriki 38 watatoka sekta bifasi na 12 kutoka Serikalini.

Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli ya Johari Rotana ambaye ni miongoni mwa waandaaji wa tuzo hizo katika upande wa hoteli, Ahmed Said amesema wao kama hoteli wamejipanga vyema kuhakikisha wanawahudumia vyema wageni wote watakaofika kwenye tuzo hizo.

Naye,Mkurugenzi wa Masoko kutoka hospitali ya Shifaa Victoria Tarimo amesema wamejipanga vyema kuhakikisha wanatoa huduma za kimataifa katika kuwahudumia wageni hao ambao watapata changamoto za kiafya wakati wa tuzo hizo.

“Sisi tumejipanga vizuri na tunavifaa vya kisasa kabisa kwa ajili ya kuwahudumia na tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha tunawapa huduma nzuri kwani tunavifaa vya kisasa na wataalam wa kutosha lakini pia tutakuwa na gari la wagonjwa kwa ajili ya dharura”,amesema.

Amesema Hospitali imejipanga kusapoti agenda ya Rais Dk Samia ya Tiba utalii kwa vitendo.

Tuzo hizo zilianIshwa mwaka 1993 lengo likiwa kutambua mchango wa wadau walipo katika sekta ya utalii katika maeneo mbalimbali Duniani ambapo sasa zinatarajiwa kufanyika june 26,2025 katika hotel ya Johari rotana  jijini Dar es salaam ambapo hoteli hiyo pamoja na hospitali ya shifaa ndio watakaohudumia watu katika Tuzo hizo.