TTCL YAKABIDHI GARI BAJAJI KUBORESHA HUDUMA YA MKONGO WA TAIFA

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

SHIRIKA  la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhi  magari tisa  aina ya Toyota Hilux yenye thamani ya zaidi ya Sh  Bilioni 1.6  bajaji nane  zenye thamani ya Sh Milioni 291 kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wananchi hasa katika mkongo wa Taifa.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL CPA Moremi Marwa  alisema ununuzi wa gari hizo ma.bajaji a ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika wa kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha utendaji kazi wa mkongo wa Taifa.

Alisema  ununuzi wa vitendea kazi hivyo unatokana na faida iliyopatikana ndani ya shirika, na kwamba hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kuboreka kwa kasi na ufanisi zaidi.

“Magari haya tisa aina ya Toyota Hilux yatasaidia shughuli za kuhudumia mkongo wa taifa. Mafundi wetu watakuwa na uwezo wa kufika haraka maeneo yenye changamoto kama kukatika kwa fiber au hitilafu nyingine ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora wakati wote,” alisema CPA Marwa.

Aliongeza kuwa bajaji 28 zilizonunuliwa zitasaidia kusogeza huduma za “fiber mlangoni kwako” kwa wananchi hasa katika maeneo ya mijini ambapo mahitaji ya huduma za intaneti yanaongezeka kwa kasi.

“Tunataka kuwafikia wateja wetu kwa karibu zaidi,bajaji hizi zitasaidia mafundi na timu za biashara kufika kwa haraka maeneo yenye changamoto na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa,” alieleza.

Mbali na magari hayo, TTCL pia imenunua magari ya biashara aina ya Hiace yatakayosaidia wafanyakazi wa shirika kuwafikia wateja wapya na kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini bila changamoto za usafiri.

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa uwekezaji huo umetokana na mafanikio ya kifedha yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika ulioanza mwaka jana.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025, TTCL ilikusanya mapato yaliyofikia takriban Sh Bilioni 229 na kupata faida ya karibu Sh Bilioni 23. Sehemu ya faida hiyo imeelekezwa serikalini, nyingine katika kuendeleza miundombinu ya mawasiliano, huku sehemu ikitumika kununua vitendea kazi hivyo.

“Katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 mpaka sasa tumeshafikia karibu bilioni 19 za faida kabla ya kufunga mwaka wa fedha mwezi Juni. Tunategemea kuvuka faida ya bilioni 23 tuliyoipata mwaka uliopita,” alisema.

Aidha, TTCL imeendelea kutekeleza mradi wa “Fiber Mlangoni Kwako” katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Mbeya, Zanzibar na Arusha.

Kwa mujibu wa shirika hilo, lengo ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za intaneti ya kasi kwa kujenga miundombinu kwanza kabla ya wateja kuomba huduma.

“Mpango wetu ni kufikia maunganisho 280,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha. Hadi sasa tumefikia karibu maunganisho 200,000 na tunatarajia kufikia lengo hilo katika robo ya mwisho ya mwaka,” alisema.

Alibainisha TTCL pia imeweka malengo ya kufikia maunganisho milioni moja ndani ya miaka mitatu ijayo kama sehemu ya kuendelea kupanua huduma za mawasiliano nchini.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa  TTCL Mhandisi Cecil Francis, alisema kuwa ununuzi wa vitendea kazi vipya ni sehemu ya jitihada za shirika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kuboreshwa kwa wananchi kote nchini. 

Alisema licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mawasiliano duniani, TTCL imeendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa vya kisasa ili kuwahudumia wateja wake kwa ufanisi zaidi, hususan wanaotumia huduma za mkongo wa taifa na huduma za “Fiber Mlangoni Kwako”.

Mhandisi Francis alieleza kuwa kwa niaba ya wafanyakazi wa TTCL, wanaahidi kutumia vifaa hivyo kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha changamoto za mawasiliano zinatatuliwa kwa haraka na huduma zinaendelea kuwa bora zaidi.