DMI:WATALAAMU WA USAFIRISHAJI MUHIMU KUONGEZA USHINDANI WA BIDHAA ZA NDANI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHUO cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesema kuwa Tanzania inahitaji kuongeza idadi ya wataalamu wa usafirishaji na usimamizi wa mnyororo wa bidhaa ili kuongeza tija, ushindani wa bidhaa za ndani na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza wakati wa alipotembelea Maonesho ya Wakulima Nanenane ,Mkuu wa chuo cha DMI, Dk. Tumaini Gurumo,amesema kuwa pamoja na chuo hicho kujulikana zaidi kwa kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari na mabaharia, kinatoa pia mafunzo ya lojistiki na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, eneo ambalo ni muhimu katika kukuza biashara.

Dk. Gurumo amesema kilimo na shughuli za bahari haziwezi kutenganishwa kwa kuwa mazao yanayozalishwa nchini yanahitaji mifumo bora ya usafirishaji ili kuwafikia walaji na masoko kwa wakati.

“Tunapozungumzia biashara shindani, tunahitaji wataalamu katika maeneo mbalimbali, likiwemo hili la lojistiki za usafirishaji wa mazao, mifugo, abiria na bidhaa nyingine,” amesema.

Amesema endapo Tanzania itaongeza uzalishaji wa mazao bila kuwa na wataalamu na mifumo bora ya kuyasafirisha, juhudi hizo zinaweza kukosa tija kutokana na changamoto za kuyafikisha mazao katika masoko kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika.

Kwa mujibu wa Dk. Gurumo, uwepo wa wataalamu wenye ujuzi katika mnyororo wa usafirishaji ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa, kwani ushindani wa kiuchumi hauishii ndani ya mipaka ya nchi.

“Tunapozungumzia biashara shindani au uchumi shindani, maana yake si kushindana ndani ya nchi pekee, bali tunautazama ushindani wa kimataifa,” amesema.

Amesema DMI imeendelea kuboresha mitaala yake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na akili bandia (AI) katika sekta ya usafirishaji.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wahitimu wanaingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya usafirishaji na uchumi kwa ujumla.

“Tunapotengeneza mitaala yetu tumeibadilisha na sasa kila mtaalamu mpya anahusisha masuala ya kidijitali pamoja na AI,” amesema.

Mbali na maboresho ya mitaala, amesema chuo hicho kimeongeza na kuboresha vifaa vya kufundishia ili wanafunzi wapate ujuzi unaoendana na teknolojia zinazotumika katika sekta husika.

Dk. Gurumo amesema DMI pia inashirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya usafirishaji na viwanda ambako wahitimu wake huenda kufanya kazi, hatua inayosaidia chuo kufahamu mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira.

Amesema ushirikiano huo pia unawapa walimu nafasi ya kujifunza teknolojia mpya na kuzitumia katika kuboresha mitaala pamoja na vifaa vya kufundishia.

Katika maonesho hayo, amesema DMI imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na vijana kuhusu fursa za mafunzo zinazotolewa na chuo hicho, akiwataka vijana kuzitazama sekta za bahari, usafirishaji na lojistiki kama maeneo yenye fursa za ajira na kujiajiri.

“Tunatambua kwamba vijana wamechukua sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini. Lazima wapate elimu na ujuzi na wajue kwamba kuna sekta ambazo wana uwezo wa kuzifanyia kazi na kupata weledi utakaowasaidia kupata ajira na kupeleka maendeleo ya nchi yetu mbele,” amesema.