TBA YAANZA SAFARI YA KUCHOCHEA UCHUMI KUPITIA MIRADI YA UWEKEZAJI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeweka mkakati wa kuchochea shughuli za kiuchumi nchini kwa kuwashirikisha wawekezaji katika ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara, viwanda na miundombinu ya kuhifadhi na kuchakata mazao.

Hatua hiyo inatajwa kuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao, kufungua masoko mapya kwa wakulima na wafugaji pamoja na kuongeza shughuli za biashara na ajira katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, amesema taasisi hiyo imepanua wigo wa shughuli zake baada ya sheria yake kufanyiwa marekebisho Agosti 2023, hatua iliyowezesha ushirikiano mkubwa zaidi na sekta binafsi.

Amesema TBA imefanya upembuzi yakinifu katika maeneo zaidi ya 147 nchini ambayo yanaweza kutumika kwa miradi ya uwekezaji, huku maeneo 38 yakiwa tayari yametangazwa kwa ajili ya kuwapokea wawekezaji.

Kwa mujibu wa Lumuli, fursa hizo zinahusisha ujenzi wa nyumba za makazi, vituo vya biashara, viwanda pamoja na miundombinu inayolenga kuongeza shughuli za uzalishaji na biashara katika maeneo husika.

Amesema TBA pia inalenga kutumia utaalamu wake wa ujenzi kusaidia kuboresha miundombinu ya sekta ya kilimo na ufugaji, hususan maghala na vituo vya kuhifadhi mazao.

“Tunafahamu ili kilimo kiwe na tija na mkulima aweze kupata thamani ya kile alichowekeza, lazima awe na sehemu nzuri na salama ya kuhifadhia mazao,” amesema.

Amesema uwekezaji katika miundombinu ya kuhifadhi, ikiwemo yenye mifumo ya ubaridi, unaweza kupunguza uharibifu wa mazao na kuongeza muda wa bidhaa kufika sokoni zikiwa katika ubora unaotakiwa.

Ametaja bidhaa zinazoweza kunufaika na miundombinu hiyo kuwa ni samaki, nyama, mboga na matunda, ambazo zinahitaji mazingira maalumu ya uhifadhi ili kudumisha ubora wake.

Kwa mujibu wa TBA, uwekezaji huo unaweza kumwezesha mkulima na mfugaji kupata thamani zaidi ya bidhaa zao badala ya kuuza mazao ghafi kwa bei ndogo kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhi na kuchakata.

Lumuli amesema TBA pia inawakaribisha wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao katika maeneo hayo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya bidhaa na kuchochea shughuli za viwanda nchini.

Ametoa mfano wa mahindi ambayo mkulima anaweza kuuza yakiwa yamechakatwa kuwa unga, huku mpunga ukichakatwa na kuuzwa kama mchele, hali inayoweza kuongeza thamani ya bidhaa na fursa za biashara katika mnyororo wa uzalishaji.

Amesema kwa kuunganisha uwekezaji wa majengo, viwanda na miundombinu ya kilimo, TBA inalenga kutumia maeneo hayo kama kichocheo cha shughuli za kiuchumi na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi.

TBA imesema iko tayari kushirikiana na wawekezaji, wakulima, wafugaji na Watanzania kwa ujumla katika kuendeleza miradi yenye tija, kuongeza thamani ya mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi.