PROFESA KABUDI AWAAHIDI NIC KUWAPA MIRADI YA MICHEZO

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaa

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amelitaja Shirika la Bima Taifa (NIC)kuwa ni miongoni mwa mashirika yanayostahili kupewa miradi ya kuendeleza mambo mbalimbali yakimichezo kutokana  na kudhihirisha uwezo wao katika usimamiaji wa miradi mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam wakati,akipokea ombi kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa NIC,Karim  Meshack juu ya NIC kupata nafasi ya kuendesha miradi ya sekta ya michezo ikiwemo ujenzi wa Viwanja mbele ya waziri huyo alipotembelea katika banda la shirika hilo lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika jijini Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.

Alisema kutokana na kasi hiyo NIC inaweza kupewa miradi ya ujenzi wa viwanja,kwasaabu ya uwezo waliokuwa nao na sio kukabidhiwa kwa sababu ni shirika la Umma.

”Sio suala  la upendeleo bali mnastahili kwa uwezo mlionao na tayari mmeingia katika high score na hilo ni muhimu sana kwa mashirika yote ya umma kwenda kwenye high score,”alisema.

Aidha alilipongeza Shirika hilo kwa kuunga mkono katika idara yake na sekta ya michezo kwa ujumla kwa kuwa wadhamini wakuu katika mashindano mbalimbali ikiwemo Mapinduzi Cup,timu ya Yanga pamoja na Pamba Cup.

”Nashukuru sana kwa kushajiisha sekta ya michezo  na kuwa wadhamini wa Klabu zote  ya Mapinduzi Cup,Pamba Cup na Yanga Fc hii ni moja ya kuonesha ni namna gani mpo vizuri hata katika sekta ya michezo,”alisema .

Kwa Upande wake Mkurugenzi  huyo Meshack alisema NIC ni Shirika pekee la Serikali linalounga mkono Idara na Sekta  ya Michezo na kuwa wadhamini katika mashindano mbalimbali ikiwemo Mapinduzi Cup.

”Hii ni dhamira ya NIC kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Idara hiyo na kutoa hamasa kwa wachezaji wanaoshiriki michuano mbalimbali kufanya vizuri zaidi katika michezo,”alisema.