TMX YAUZA KAKAO YENYE THAMANI YA SH BILIONI 3.7 NANE NANE

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

SOKO la Bidhaa Tanzania (TMX) limefanikiwa kuuza kakao yenye thamani ya shilingi billioni 3.7 katika maonesho ya NaneNane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma.

Akitoa taarifa hiyo leo, Afisa Masoko wa TMX, Bi. Shanny Mringo, amesema kuwa jumla ya tani 255 za kakao zimeuzwa kupitia mfumo huo wa kidigitali kwa bei ya shilingi 14,520 kwa kilo.

Amebainisha kuwa fedha hizo zimeelekezwa moja kwa moja kwa wakulima, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa mkulima ananufaika moja kwa moja na jasho lake bila vikwazo vya madalali.

“Kupitia TMX, tunahakikisha kuwa bidhaa za wakulima zinafikia masoko kwa njia ya uwazi, salama, na yenye faida kwao.

Tunajivunia kuona kuwa leo tumefanikisha mauzo ya kiwango hiki cha juu kwa bei nzuri inayomfaidisha mkulima,” amesema Bi. Mringo.

Wakulima waliotembelea banda la TMX katika maonesho hayo wamepongeza mfumo huo kwa kusaidia kuuza mazao yao kwa uwazi, bila udanganyifu na kwa bei yenye ushindani.

Mfumo wa TMX unaendelea kuimarika kama jukwaa muhimu katika kuleta mageuzi ya masoko ya mazao nchini, huku serikali na wadau mbalimbali wakihamasisha wakulima wengi zaidi kujiunga na kutumia mfumo huo ili kunufaika na fursa zilizopo katika soko la kisasa la bidhaa.