Na Asha Mwakyonde, DODOMA
KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali kupunguza migogoro ya kisheria miongoni mwa wananchi, Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutoa huduma katika maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, ametoa pongezi kwa Wizara hiyo baada ya kutembelea banda lao Agosti 6, 2025, ambapo alieleza kuwa uwepo wa Wizara hiyo katika maonesho hayo ni hatua muhimu katika kusaidia wananchi kutatua migogoro mbalimbali, hasa ya ardhi, ambayo bado imeendelea kuwakabili wengi katika mkoa wa Dodoma.

“Huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa kupitia Kampeni ya Mama Samia ni msaada mkubwa kwa wananchi, hasa wale wa kipato cha chini. Migogoro mingi ya ardhi inaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia elimu na usaidizi wanaoupata hapa,” amesema Shekimweri.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika banda hilo ili kuwasilisha malalamiko na kupata ufumbuzi wa changamoto zao kutoka kwa wataalamu wa sheria waliopo katika eneo hilo.

“Nimefurahi kuona kuwa huduma hii haishii tu kwenye usuluhishi, bali pia wananchi wanapewa elimu ya kisheria. Kinamama wanapaswa kujitokeza kwa wingi, hasa kwa ajili ya kujifunza kuhusu masuala ya mirathi ambayo mara nyingi wao ndio waathirika wakubwa,” ameeleza.
Aidha ,Shekimweri amepongeza juhudi za Wizara katika kutoa elimu ya Haki na Utawala Bora, akieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

“Tunaelekea katika kipindi cha uchaguzi, na elimu inayotolewa hapa itawasaidia wananchi kutambua haki na wajibu wao, jambo litakalowawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia,” amesisitiza.


