Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
AFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Mkama Bwire amefanya ziara ya kikazi kukagua hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ubungo na Ilala katika maeneo ya Ubungo, Mburahati, Magomeni, Saranga na Kinyerezi.
Ziara hiyo ililenga kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji na kutafuta suluhisho katika maeneo yenye changamoto za kihuduma zinazowakabili wananchi.

“Huduma ya Maji katika eneo letu la kihuduma Dar na Pwani iko vzr na leo tunapita mitaan kukagua na kujiridhisha upatikanaji wa huduma tunayozalisha kama inawafikia wananchi na iwapo kama kuna changamoto basi tunazitatua na wananchi wanaendelea kufurahia huduma” alisema Mhandisi Bwire
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kinyerezi Ndugu Hassan Hamiss Nandeta, aliishukuru DAWASA kwa hatua madhubuti ilizochukua katika kuboresha huduma ya maji safi kwenye maeneo yao, akibainisha kuwa wananchi wameanza kunufaika na maboresho hayo.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea kutekeleza mkakati wa kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora na ya uhakika.
