Na Aziza Masoud, Dodoma
WAZIRI Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupanua huduma za utoaji wa mikopo kwa lengo la kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi nchini ili kuweza kusaidia uwekezaji katika sekta ya uzalishaji na kuharakisha mageuzi.
Dk.Mwigulu ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika Maonesho ya Taifa ya Wakulima Nanenane baada ya kutembelea banda la benki ya TADB na kuwa benki hiyo imeendelea kuwa chombo muhimu cha Serikali katika kuwezesha uwekezaji kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutoa mitaji kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji mbalimbali.

Alisema hatua hiyo iende sambamba na kujiimarisha katika uwezo wa kifedha kwa lengo la kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi nchini ambapo itasaidia kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji.
Alisema pia itasaidia kuharakisha mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza tija na uzalishaji, sambamba na kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta hizo zinazobeba maisha ya Watanzania wengi.

Alisema ili Tanzania ifikie malengo ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula nchini, kuna umuhimu wa kuendelea kuiwezesha TADB kifedha ili iweze kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo.
” Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka katika kuendeleza sekta ya kilimo, hivyo taasisi za kifedha kama TADB zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha mitaji inapatikana kwa wakati kwa wakulima, wafugaji na wavuvi,”alisema Dk.Nchemba.

Alisema kuwa benki hiyo inapaswa kuongeza uwezo wa kufadhili ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao ili kuongeza tija, ushindani na thamani ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki ya TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi mbalimbali ya kimkakati inayochochea ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Amesema zaidi ya Sh Bilioni 700 zimetolewa kufadhili miradi ya umwagiliaji, huku zao la kahawa kutoka mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia vyama vya ushirika likitajwa kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyowavutia wadau wengi waliotembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane.
Ameongeza kuwa TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri, wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi, huku ukizingatia uhifadhi wa mazingira na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema uwekezaji huo umechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mchango wa sekta za kilimo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.


