REA, TANESCO WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUONGEZA IDADI YA WATEJA VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu,Arusha

MWENYEKITI wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, ametoa rai kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutoa kifaa maalum (Ready boards) ambacho kitawezesha wananchi kusaidia kupunguza gharama kubwa za kuunganisha mfumo wa kupokelea umeme nyumbani (wiring) kwenye miradi ya umeme vijijini.

Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amebainisha hayo leo Novemba 16, 2025 wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA mkoani Arusha..

Amesema kifaa hicho kitasaidia kuongeza idadi ya wateja na kuwarahisishia wananchi kuepuka gharama kubwa wanazotumia kwenye kuweka mfumo wa kupokelea umeme majumbani kwenye miradi ya umeme vijijini.

Katika hatua nyingine, ametoa rai kwa menejinti ya REA kukutana na kuzungumza mara kwa mara na wadau ili kupata maoni ya kuwezesha kufikia malengo (Maadhimio) yaliyopaangwa kwenye Mkutano wa M300 uliofanyika hapa nchini.

Aidha ameelekeza wasimamizi wa miradi kuongeza juhudi kwenye usimamizi wa karibu wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa huu kwa kasi zaidi ikiwa na lengo la kuwapatia huduma za nishati wananchi wote ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchuni katika maeneo hayo ya vijijini,” Amesema Mhe. Balozi Kingu.

Vile vile amesema kuwa, vitongoji 965 sawa na asilimia 64.12 kati ya vitongoji 1,505 vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), iliyopita na inayoendelea kutekelezwa katika mkoa wa Arusha.

Ameeleza kuwa, mkoa wa Arusha una jumla ya vijiji 368 ambapo vijiji vyote 368 sawa na asilimia 100 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA iliyotekelezwa katika mkoa huo.

Katika hatua nyingine amewataka Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA, kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake, Mhandisi Miradi wa REA mkoa wa Arusha, Mha. Darwin Eradius amesema kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Wakala wa kufikisha umeme kwa wananchi wote nchini.

“Katika mkoa huu jumla ya miradi miwili ya kusambaza umeme vitongojini inatekelezwa ambayo ipo katika hatua za utekelezaji ukiwemo mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji awamu ya pili A (HEP 2A), na Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B (REDP IIB).

Halikadhalika, Serikali kupitia REA imetoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 79.6 ili kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa mkoani humo na wananchi wanapatiwa huduma ya umeme ili kuwapatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Fedha hizo zimetolewa na Serikali ili kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi” Amesema Mha. Eradius.

Kwa upande wa Wakandarasi hao wa miradi kwa ujumla wamemshukuru Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha REA kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati ya umeme vijini mkoani Arusha hali inayokwenda kuchochea maendeleo kwa ujumla.

Wakandarasi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na mkandarasi Ceylex Engineering (Pvt) Ltd, na Urban and Rural Engineering Services Ltd.