Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Yusuph Mwenda ameitaka jamii kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kukamilisha ndoto zao na kufikia malengo waliyojiwekea.
Kamisha Mwenda ametoa kauli hiyo wakati akitoa msaada kama sehemu ya kuadhimisha mwezi wa mlipa kodi katika vituo vyakulelea watoto yatima cha Hisani kilichopo Kigamboni pamoja na kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili Deconia kilichopo mtoni kilicho chini ya Kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania (KKKT) kilichopo Mtoni.

Alisema jukumu la kuwatunza watoto wenye mahitaji maalum ni la jamii nzima hivyo kila mwananchi mwenye uwezo anapaswa kujua jinsi gani ataweza kuchangia mahitaji ya watoto.
“Sisi kama TRA tupo kwenye mwezi wa kuwashukuru walipa kodi ambao ni Desemba,misaada hiyo inayotolewa imetokana na michango ya walipa kodi waliyochangia kwa serikali,jukumu lakutunza watoto wanaoishi katika kundi hili ni letu sote,natoa wito kwa jamii kuendelea kulisaidia kundi hili kwakuwa vituo pekee haviwezi kuwatosheleza,”alisema Kamishna Mwenda.
Alisema watoto hao pamoja na kwamba wanalelewa katika vituo hivyo lakini wana ndoto zao ndiyo maana wapo wanaopambana kusoma na kufikia viwango mbalimbali vya elimu ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Awali Msimamizi Mkuu wa kituo cha Deconia Winfrida Malumbo alisema alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1984 kutoa huduma kwa watoto wenye ulemavu wa akili kwa usimamizi wa kanisa la KKKT.

Alisema kituo kimekuwa na programu mbambali ambapo kupitia mifumo hiyo wanalea watoto wenye umri kuanzia miaka mitatu mpaka miaka kumi.
“Kupitia programu zetu tuna huduma mbalimbali zakuweza kuwainua watoto zikiwemo za kulea watoto majumbani,kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi kumi,kupitia programu hii mzazi anajifunza jinsi yakumtunza mtoto mwenye ulemavu nyumbani,”alisema Malumbo.

Alisema programu nyingine ni elimu maalum kwa ajili ya watoto wenye ulemavu kwa ushirikiano mzuri kati ya serikali na kanisa pamoja na huduma ya matendo ya huruma kwa wahitaji.
Alisema watoto hao kuwatunza ni gharama kuwatunza watoto hao kwenye masuala ya matibabu na milo kamili ni kubwa hivyo kunahitaji msaada wa watu kutoka nje.
Naye mmiliki wa kito cha kulelea yatima cha Hisani kilichopo Kibada Kigamboni Hidaya Mutalemwa alisema kituo hicho kilianzishwa Mei 2005 mpaka sasa kiba watoto 91 ambapo kinalea watoto kuanzia miaka miwili mpaka vyuo vikuu kwa lengo kuwasaidia kundi hilo lenye uhitaji.

Alisema pamoja na kutoa huduma hizo kituo hicho kinachangamoto mbalimbali ikiwemo usafiri,huduma ya bima kwa watoto pamoja na chakula kutokana na wingi wa watoto.


