Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
MWAKA 2025 umeandika historia mpya kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato, upanuzi wa wigo wa kodi, na uimarishaji wa mahusiano kati ya TRA na Walipakodi. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mwelekeo mpya wa utoaji huduma unaolenga ushirikishwaji, elimu, na ulipaji wa kodi kwa hiari badala ya matumizi ya nguvu.
Mwaka 2025 umeonesha TRA kuwa karibu zaidi na Walipakodi. Kupitia ziara za mara kwa mara katika maeneo ya biashara, TRA imeweza kusikiliza changamoto za Walipakodi moja kwa moja, kuzitatua kwa wakati, na kutoa elimu sahihi ya kodi. Hatua hii imeongeza imani kwa Walipakodi na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari, hali iliyoleta matokeo chanya katika makusanyo ya mapato ya Serikali.

Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara: TRA Kugusa Maisha ya Wananchi
Moja ya alama muhimu za mafanikio ya TRA mwaka 2025 ni kuanzishwa kwa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara, mpango ulioleta mabadiliko ya kweli kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini. Dawati hili lilizinduliwa rasmi Agosti 2025 mkoani Morogoro na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, ambaye alitoa agizo la wazi kwamba kila mkoa nchini uwe na dawati hilo, agizo ambalo tayari limetekelezwa kikamilifu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenda alisema:
“Dawati hili litatatua changamoto za Walipakodi na kutoa ushauri wa biashara na mikopo ili kuwezesha ustawi wa biashara nchini; kila mkoa unapaswa kuwa na dawati hili.”
Kupitia dawati hili, wafanyabiashara wamepatiwa elimu ya biashara, elimu ya masuala ya mikopo, ushauri wa kitaalamu, pamoja na kuwezeshwa mitaji. Katika hatua ya kuonesha dhamira ya dhati, Kamishna Mkuu alitoa mitaji kwa baadhi ya vikundi vya wafanyabiashara karibu katika mikoa yote.
Miongoni mwa wanufaika ni Mussa Amiri, mkazi wa Dar es Salaam, ambaye kikundi chao cha ujasiriamali kilipatiwa mtaji wa Shilingi milioni 2. Mussa anasema fedha hizo zimewawezesha kupanua biashara yao ya nguo kwa kuongeza bidhaa na kuvutia wateja wengi zaidi.

“Tunamshukuru sana Kamishna Mkuu wa TRA. Mwaka 2025 amegusa maisha yetu. Tulikuwa na mtaji mdogo lakini sasa idadi ya wateja imeongezeka na biashara inakua,” anasema Mussa.
Naye Anna Bakari kutoka mkoani Geita anashuhudia namna uwezeshaji huo ulivyobadilisha maisha yao. Anasema biashara yao ya chakula ilikuwa imeyumba na kufungwa kutokana na ukosefu wa mtaji, lakini baada ya kuwezeshwa na TRA, wameanza upya kwa mafanikio.
Kupitia Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara, Anna na wenzake walipata elimu ya biashara, wakapatiwa TIN bure, hatua iliyowawezesha kupata leseni ya biashara kutoka Halmashauri na kurasimisha shughuli zao. Kwa sasa, biashara yao inatambulika kisheria na wana mipango ya kuanza kulipa kodi.

Anna anatoa wito kwa wananchi na Walipakodi wote:
“Natoa wito kwa wananchi kutembelea dawati la uwezeshaji biashara ili kupata elimu ya biashara na kodi; huduma hizi zinabadilisha maisha.”
Uzinduzi wa Ofisi za TRA
Katika mwaka 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua jingo la kisasa la ofisi za TRA mkoa wa Simiyu sambamba na majengo mengine yote ambayo ujenzi wake ulikuwa umekamilika na kuwataka watumishi wa TRA kuendelea kutoa huduma bora.
Rais Samia alisema majengo hayo ni kwaajili ya kuwahudumia Watanzania na kuwawekea mazingira mazuri ya kulipa kodi.

“Uzinduzi wa ofisi hii unaambatana na uzinduzi wa ofisi zote mpya zilizojengwa na zilizokarabatiwa kwa nchi nzima, hivi sasa walipakodi watapatiwa huduma katika mazingira mazuri” alisema Dkt. Samia.
Upanuzi wa Wigo wa Kodi na Mageuzi ya Usajili
Katika jitihada za kuongeza wigo wa kodi, mwaka 2025 TRA ilianzisha usajili wa biashara kwa njia ya mtandao, hatua iliyoanza na wamiliki wa makazi ya kupangisha kupitia majukwaa ya Airbnb. Mpango huu umepokelewa kwa muitikio mkubwa na unatarajiwa kupanuliwa kwa wafanyabiashara wengine wa mtandaoni, wakiwemo mawakala wa usafirishaji na watoa huduma za kidijitali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Kamishna Mkuu Mwenda alisema elimu inaendelea kutolewa kwa wafanyabiashara wa mtandaoni ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ulipaji kodi.
“Iwapo tutakuwa na Walipakodi wengi, kila mmoja atachangia kwa haki, na kuna uwezekano mkubwa wa viwango vya kodi kupungua kupitia kuongeza wigo wa kodi,” alisema Mwenda.
Kongamano la Kodi na Ubunifu wa Vyanzo Vipya vya Mapato
TRA pia iliandaa Kongamano la Kodi kupitia Chuo cha Kodi (ITA), likiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi. Kongamano hilo lilijadili mikakati ya kuongeza wigo wa kodi na kudhibiti ukwepaji wa kodi.
Matokeo makubwa ya kongamano hilo ni kuzaliwa kwa:
• Tuzo ya Mtoa Taarifa, itakayotolewa kwa watakaosaidia kutoa taarifa za ukwepaji wa kodi.
• Tuzo ya Ubunifu wa Vyanzo Vipya vya Kodi, kwa lengo la kuhamasisha ubunifu katika kuongeza mapato ya Serikali.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Angelina Ngalula, alipendekeza kuwepo kwa mfumo mmoja wa usajili wa wafanyabiashara unaojumuisha Halmashauri, BRELA na TRA.

“Nashauri kuwepo kwa mfumo mmoja wa usajili wa wafanyabiashara; usajili ufanyike bure, kodi itapatikana baadaye,” alisema Bi. Ngalula.
Ajira, Ufanisi wa Makusanyo na Rekodi Mpya
Mwaka 2025 pia umeandika historia kwa TRA kuajiri watumishi zaidi ya 1,800 wa kada mbalimbali — idadi kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo. Hatua hii inalenga kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa elimu ya kodi.
Kwa upande wa makusanyo, TRA imevunja rekodi zake yenyewe. Katika mwaka wa fedha 2024/25 (Julai 2024 – Juni 2025), TRA ilikusanya Shilingi trilioni 32.26, sawa na asilimia 103.9 ya lengo la Shilingi trilioni 31.05, na ukuaji wa asilimia 16.7 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka uliopita ya Shilingi trilioni 27.64.

Aidha, katika robo ya nne pekee (Aprili–Juni 2025), TRA ilikusanya Shilingi trilioni 8.22, sawa na ufanisi wa asilimia 104.8, ongezeko la asilimia 15.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema mafanikio haya yametokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayosisitiza ulipaji kodi wa hiari badala ya matumizi ya nguvu. Miongoni mwa hatua zilizochochea mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa Tuzo za Rais kwa Walipakodi Bora, kuundwa kwa Tume ya Maboresho ya Kodi, na uboreshaji wa miundombinu ya ofisi za TRA.
Vita dhidi ya Magendo na Mwelekeo wa 2026
Katika kufunga mwaka 2025, TRA imetangaza vita kali dhidi ya magendo, hususan uingizaji wa mafuta ya kupikia bila kufuata taratibu za forodha. Hatua hiyo ilitangazwa baada ya kukamatwa kwa madumu 18,255 ya mafuta ya kupikia ya magendo jijini Dar es Salaam.

“Tutawasaka waingizaji wa magendo wote na kuwachukulia hatua; pia ninaunda timu itakayohusisha wadau wote ili kupata suluhisho la kudumu,” alisema Bw. Mwenda.
Kwa mwaka 2026, TRA imejipanga kuendelea kuboresha huduma, kuimarisha elimu ya kodi, kusikiliza Walipakodi, na kutatua changamoto zao kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya safari ya kujenga uchumi imara unaochangiwa kwa haki na kwa hiari na Watanzania wote.
Kwa hakika, mwaka 2025 umeiweka TRA katika ukurasa mpya wa ufanisi, ubunifu na huduma kwa wananchi, ushahidi kuwa kodi ikikusanywa kwa haki na kwa ushirikishwaji, maendeleo yanakuwa ya wote.



