Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema udhibiti unaofanyika na kukamatwa kwa waingizaji wakuu wa dawa za kuelvya kumefanya bidhaa hiyo iwe adimu mtaani na kusababisha vijana wengi kuhamia kwenye uraibu wa pombe kali ambazo wanakunywa kupita kiasi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Januari 9, 2026 kuhusu mafanikio ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo amesema vijana wengi hasa waliokuwa wakitumia dawa za kulevya wamehamia kwenye unywaji wa pombe kali na wamekuwa walevi kupita kiasi.

“DCEA tumedhibiti kwa kiasi kikubwa uingizwaji wa madawa ndo maana hata wale waliokuwa wanatamba mitaani wanajiita mazungu ya unga waliokuwa wanaimbwa kwenye miziki hawapo,sasa hivi vijana wamehamia kwenye pombe,vijana wamekuwa walevi kupita kiasi na sasa ndo wapo wengi kwenye nyumba za urakabisha lakini wa dawa wamepungua sana,”alisema Kamishna Lyimo.
Amesema kazi ya mamlaka ni kudhibiti dawa na si pombe wala hakuna sheria inayokataza watu kunywa pombe lakini kutokana na ongezeko kubwa la vijana hao watatoa ushauri na elimu kuhusu madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi.

Amesema mamlaka imepunguza dawa za kulevya zilizokuwa zikiingia mtaani kwa kiasi kikubwa ambapo kwa sasa hakuna vijiwe vya watumiaji wa madawa ya kulevya kama zamani ambapo ilikuwa unajua ukienda sehemu fulani utakutana na waraibu hao wa dawa.
Amesema ili kuendelea kudhibiti na kupambana na dawa hizo DCEA itaendelea kuwajengea wa mafunzo zaidi kwa watumishi wake waweze kuwa na weledi na utii kwakuwa dawa za kuelvya zinaambatana na rushwa hivyo ni lazima kuwa na watumishi waliokuwa tayari.

Amesema pamoja na kupungua kwa dawa lakini mamlaka imeweka mkakati madhubuti kwa mwaka huu 2026 kuhakikisha wanaondoka mashamba ya bangi,mirungi pamoja na vijiwe vya wafanyabiashara hizo.

