Na Ashrack Miraji
Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameeleza kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wakazi wa Kata ya Vumari kuhujumu miundombinu ya miradi ya maji inyotekelezwa na Serikali.
Hujuma hizo ni wizi wa panel za Sola, Bomba za chuma, Kukata kata Bomba za maji za plastiki pamoja na dira za maji (mita) na kuitia hasara Serikali ya milioni 370.
Ameeleza hayo kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kizungo Kata ya Vumari ulipo mradi huo mkubwa unaohudumia wakazi wa Vijiji viwili vya Kizungo na Minyara uliotekelezwa na Serikali kupitia Benk ya Dunia.
Awamu ya kwanza katika mradi huo uligharimu shilingi Milioni 980 kisha awamu ya pili kuongezewa kiasi cha shilingi Milioni 240 ili mradi uweze kutoa huduma kwenye maeneo ya milimani ambako kunahitaji nguvu ya umeme kupandisha maji.
Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Wilayani humo kumkamata mwananchi mmoja aliyefanya vurugu kwenye kituo cha kutolea huduma ya maji (DP – Domestic Point) na kuharibu miundombinu yake akidaiwa kugoma kulipia ndoo moja ya maji aliyoenda nayo kituoni hapo kupata huduma.
“Mwananchi yeyote anayehujumu miradi ya Serikali ambayo Rais amehangaika kutafuta fedha na kutuletea kwa wanasame siwezi kumfumbia macho mtu wa namna hiyo tutamchukulia ni mharifu kama waharifu wengine”. alisema Kasilda.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA wilaya ya Same, Mhandisi. Abdallah Gendaeka amesema miongoni mwa changamoto inayokwamisha jitihada za Serikali ni pamoja na hujuma zinazofanywa na wakazi wenyewe kwenye mradi huo na kupelekea utekelezaji wake kuwa wa muda mrefu ambapo ni miaka 10 sasa tangu kuasisiwa kwake 2014.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo ambao ni wanufaika wa mradi huo bado wanaendelea kuteseka kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye mito licha ya kuwa na mradi mkubwa na kuomba Serikali iwachukulie hatua hao watu wanaohujumu miundombinu.
Kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji upande wa Same mjini hadi kufikia June 30 mwaka huu utakuwa asilimia zaidi ya 100% hii ni kutokana na kukamlika kwa mradi mkubwa wa maji Same – Mwanga – Korogwe kwa awamu ya kwanza.
Lakini pia upande wa Vijijini ni asilimia 74% sasa iliyofikiwa huku tayari Serikali katika mwaka wa fedha 2024/25 imetenga zaidi ya bilioni 2.4 kwa ajili ya miradi ya maji hivyo kufanya lengo la utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kufikiwa kwa asilimia 100% mjini na vijijini ifikapo mwezi wa Octoba 2024 baada ya miradi yote inayotekelezwa Wilayani Same kukamilika.