DK.MWIGULU:TUTAENDELEA KUWACHUKULIA HATUA KALI WANAOTOA MIKOPO ‘KAUSHA DAMU’

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam.

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha  imesema itaendelea kuchukua hatua kali kwa taasisi zote zininazotoa huduma za fedha kinyume cha sheria kwa kutoa mikopo umiza (kausha damu) na kuwakandamiza wananchii.

Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 10,2024 limetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba,wakati akizindua Jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024. 

Amesema  taasisi hizo zimekuwa zikiwaumiza wananchi kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa pamoja na kupanga njama za kuwafilisi wale ambao wanajua wazi hawatoweza kulipa mikopo hiyo kutokana na sababu mbalimbali .

“Lazima wananchi wajue kutoafautisha kati ya tasasisi rasmi na zisizo rasmi, wananchi wengi wanahisi kukopa kwenye taasisi rasmi wanahisi hawapo salama,lazima tuwaoneshe wananchi kuwa hawako salama wanapokopa kwenye taasisi zisizo rasmi badala yake tuwahamasishe wakope  benki ambapo ni salama zaidi”, amebainisha Dkt. Nchemba.

Amesema ni vema wadau wa Sekta ya Fedha wawaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia benki kupata mikopo pamoja na kutunza fedha zao kwa kuwa kutunza fedha benki ni utaratibu wa kisasa wa uendeshaji wa uchumi.

” Bado kuna baadhi ya maeneo wananchi wanaogopa kuweka fedha benki, kwa kuwa nyinyi mpo kwenye Sekta hii mshirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaeleza wananchi kuwa wasiogope kuweka fedha benki ”, amefafanua Dk.Nchemba.

Mbali na kuzionya taasisi za mikopo zisizorasmi pia alitoa rai kwa mabenki ambapo amedai kumekuwa na michezo michafu yakufilisi wakopaji kwakushirikiana na watu ambao wanahitaji kuuziwa dhamana za wateja.

Amewaagiza viongozi wa Taasisi za Fedha nchini kujiridhisha kabla ya kuruhusu watumishi na madalali wao kupiga minada ya mali za wadaiwa mikopo hiyo.

”Kuna baadhi ya maeneo hakufanyiki vizuri katika kudai mikopo, mteja amelipa mkopo wake kwa asilimia 80, amebakiza asilimia 20, anatokea mteja mwingine anapenda dhamana ya mkopo iliyowekwa, benki inaamua kupiga mnada wa muda mfupi ambao wanajua mteja hatoweza kulipa ili wamfilisi, mtu amelipa mkopo kwa asilimia 80 halafu unauza dhamana yake ili kufidia asilimia 20 ambayo hajalipia huko ni kumtia umaskini, huu sio utaratibu mzuri wa kujenga sekta ya fedha na sio utaratibu mzuri wa kujenga ustawi wa jamii”, ameongeza Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba ameziagiza benki zilizopo  kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa benki wasio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wateja kuongeza mikopo chechefu.

Awali  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba alisema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha nchini imeandaa Jukwaa la wadau wa Sekta ya Fedha ili kubadilishana mawazo na uzoefu, kupeana taarifa, kujengeana uwezo, kushirikishana katika mafanikio na changamoto na kutafuta suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazoikabili sekta ya fedha nchini.

Alisema malengo ya Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka mitatu (2020/21-2023/24) na kushirikishana mbinu bora za kiutendaji na uzoefu katika Sekta ya Fedha.

Dkt. Mwamba alisema malengo mengine ni kujadili fursa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuboresha sekta ya Fedha pamoja na kushirikishana namna bora ya kukuza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi ili kukuza na kuimarisha Sekta ya Fedha.

Aliongeza kuwa Jukwaa hilo pia linalenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa Sekta ya Fedha na kuufahamisha Umma juu ya hatua za maboresho mbalimbali ya kisera na kisheria yaliyofanyika ili kuimarisha Sekta ya Fedha nchini.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *