Na Mwandishi Wetu,Tanga
BANDARI ya Tanga imeandika historia mpya katika ukusanyaji mapato baada ya kukusanya kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 100 ndani ya miezi mitano ikiwa ni matokeo ya uboreshaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mapato hayo yanajumuisha sh. bilioni 57 za mapato ya kodi yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na sh. bilioni 38.53 zilizokusanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mkoani Tanga ambayo inasimamia bandari hiyo.
Katika kipindi hicho, pia Bandari ya Tanga imefanikiwa kuhudumia meli 172 ikijumulisha meli 65 za bahari kuu na meli 167 za mwambao, zaidi ya lengo la kuhudimia meli 90 kwa mwaka.
Akizungumza wakati alipotembelea bandari hiyo , Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji wa sh. bilioni 429 uliofanywa katika kuboresha gati.
“Matokeo yameonekana, ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo gharama za uwekezaji zitakuwa zimesharudi. Ajira zimeongezeka kwa sababu watu wanafanyakazi muda wote,” alibainisha.
Profesa Mbarawa alieleza kuwa serikali ina mpango wa upanuzi wa magati mawili kwa mita 300 na mita 50 ambapo jumla itakuwa mita 750.
Alibainisha kuwa upanuzi huo utawezesha kuongezeka kasi ya ukusanyaji mapato kutokana na huduma zitakazotolewa, kufikia wastani wa sh. bilioni 400 hadi 500 kwa mwaka.
“Uwekezaji huu unatekelezwa katika bandari zote. Bandari zote zitaunganishwa na miundombinu ya kisasa ya reli hatua ambayo itaongeza kasi ya uteremshaji na ushushaji mizigi.
“Bandari ya Dar es Salaam imeshaungwanishwa na reli ya MGR, reli ya TAZARA na sasa mfumo unajengwa kuunganisha na reli ya SGR, Bandari ya Mwanza imeshaunganishwa na MGR lakini pia itaunganishwa na SGR,” alisisitiza.
Kuhusu Bandari ya Pangani, alisema bandari hiyo ni muhimu kwa kusafirisha mazao ya misitu, chakula na mafuta ya kupikia kati ya Unguja, Pemba na Wilaya ya Pangani.
Alieleza kuwa bandari hiyo mwaka jana ilikusanya mapato ya sh. milioni 240, lakini baada ya maboresha kwa muda wa miezi mitano mapato ya sh. milioni 124 yamekusanywa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, alisema maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo yamechochea ongezeko la ajira zaidi ya 19,000 kwa vijana wakiwemo wanawake waendesha mitambo.
Alisema katika kuongeza ufanisi wa bandari hiyo, ofisi yake inashirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutafuta miundombinu wezeshi kama maeneo ya bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo.
Pia, alisema wametenga eneo maalum litakalotumika kushusha bidhaa hatarishi huku wakiendelea kuweka mikakati kuhakikisha bandari hiyo inahudumia mazao ya chakula kama korosho kutoka mkoani Pwani, kahawa na parachichi.
Vilevile, alibainisha kuwa urasimishaji bandari bubu hususan wilayani Pangani pia umesaidia kuongeza mapato na kudhibiti biashara za magendo.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandishi Juma Kijavara, alisema mpango wa kuongeza gati katika Bandari ya Tanga utaongeza idadi ya meli zitakazohudumiwa.
Alisema gati itakayojengwa kwa mita 300 itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli tatu za mita 20O huku upanuzi wa gati nyingine kwa mita 50 utahusisha eneo la kuhudumia meli za abiria kutoka Zanzibar na sehemu ya kupumzikia.