MRADI WA MAJI CHALINZE WAMKOSHA WAZIRI KUNDO, ATOA MAAGIZO

Na Mwandishi Wetu,Bagamoyo

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ametembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo unaonufaisha zaidi ya wakazi 200,000 wa Mji wa Chalinze.

Akizungumzia na wakazi wa Kata ya Msata alipotembelea moja ya vizimba vinavyohudumia wakazi wa eneo hilo, Naibu Waziri Kundo ameipongeza DAWASA kwa kazi nzuri ya usimamizi wa mradi na kuagiza kazi chache zilizosalia zikamilishwe kwa wakati.

“Nichukue nafasi hii kuwaagiza DAWASA, kuna baadhi ya vizimba vilivyojengwa wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huu na sasa havitoi maji, mkavirekebishe na wananchi wapate huduma, lakini pia katika awamu hii ya tatu ya mradi mkandarasi ahakikishe vizimba vyote vinatoa maji kabla ya kukabidhi mradi huu,” amesema Mhandisi Kundo.

Kundo amesema kwakuwaomba wananchi kuilinda miundombinu ya maji kwa wivu mkubwa ili thamani ya fedha iliyotumika iendelee kuonekana.

“Sisi Wizara ya maji hatutakaa ofisini, tutatoka kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa ipasavyo na wananchi wanapata huduma ili adhima ya Mhe. Rais ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani iweze kukamilika,” amesema Mhandisi Kundo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga amemshukuru Naibu Waziri kwa ziara yake mkoani Pwani kwani imekuwa ya mafanikio na wanabaki na imani kubwa huduma ya maji katika maeneo ya Bagamoyo na Chalinze inakwenda kuimarika zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *