Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Mchambuzi wa masuala ya siasa, jamii na maendeleo, Habibu Mchange, ametoa tafakuri kuhusu utata wa kauli za mara kwa mara za Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, akisema kutokana na nafasi yake ya kikatiba kama Msaidizi Mkuu wa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 47(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kauli zake zinapaswa kupimwa kwa uzito mkubwa kwa kuwa zina athari kwa Serikali, mshikamano wa uongozi na imani ya wananchi kwa taasisi za dola.
Katika tafakuri hiyo yenye kichwa “DK. NCHIMBI ANAJUA MADHARA YA KAULI ZAKE AU ANATUTEGA?”, Mchange amechambua kauli ya Dk. Nchimbi kwamba “Katiba iliyopo ina mapungufu na inampa Rais madaraka yasiyo na maana,” pamoja na wito wake wa “komaeni, pambaneni mpate Katiba mpya,” akisema kauli hizo zimezua mjadala mkubwa wa kikatiba na kisiasa, hasa wakati Serikali tayari imeeleza kuwa mchakato wa Katiba mpya utaanza baada ya kukamilika kwa maridhiano ya kitaifa.
Amehoji kuwa iwapo Serikali tayari ina utaratibu huo, kauli ya kuwataka wananchi “wapambane” inazua swali la msingi; wananchi wapambane dhidi ya nani? Je, dhidi ya Serikali ambayo yeye mwenyewe ni sehemu yake, dhidi ya Rais ambaye yeye ni Msaidizi wake Mkuu, au dhidi ya Katiba aliyoapa kuilinda na kuitetea?
Mchange amesema tafakuri yake pia imejengwa juu ya kanuni ya uwajibikaji wa pamoja wa Serikali (Collective Responsibility), ambayo inawataka viongozi wakuu wa Serikali kuzungumza kwa sauti moja kuhusu sera na maamuzi ya Serikali.
Kwa mtazamo wake, Makamu wa Rais anapaswa kuwa sehemu ya kutoa majibu kwa wananchi badala ya kauli zinazoweza kuibua tafsiri tofauti kuhusu mshikamano wa Serikali, akiongeza kuwa tangu Dk. Nchimbi aapishwe amekuwa akitoa kauli ambazo mara kwa mara zimezua mijadala katika medani ya siasa.
Amesisitiza kuwa tafakuri hiyo hailengi kupinga mjadala wa Katiba mpya, bali kufungua mjadala mpana kuhusu wajibu wa viongozi wakuu wa nchi kupima athari za kauli zao kwa Taifa, kulinda mshikamano wa Serikali na kuhakikisha kila tamko lao linaendana na hadhi ya ofisi wanazoshikilia, akisisitiza kuwa viongozi wa ngazi ya Makamu wa Rais hupimwa si kwa dhamira zao pekee, bali pia kwa athari za maneno yao kwa Serikali, Taifa na wananchi.


