KAMATI YA JTC YAJIFUNZA MFUMO WA SCADA PBPA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kamati ya Pamoja ya Kiufundi (JTC) ya mradi wa Bomba Jipya la TAZAMA, inayoundwa na wataalamu kutoka Tanzania na Zambia, imetembelea Ofisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) jijini Dar es Salaam leo, Septemba 16, 2026, kwa lengo la kujifunza kuhusu usimamizi wa shughuli za upokeaji na ushushaji wa bidhaa za mafuta nchini.

Katika ziara hiyo, wataalamu hao walitembelea chumba cha uendeshaji wa Mfumo wa SCADA na kupata maelezo kuhusu namna PBPA inavyotumia mfumo huo kufuatilia mwenendo wa mafuta kutoka melini hadi kwenye matanki ya kuhifadhia.

Akiwakaribisha wageni hao, Meneja wa Mipango ya Mafuta wa PBPA, Bw. Gilbert Jungulu, alisema ziara hiyo imetoa fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu usimamizi wa shughuli na miundombinu ya mafuta.

“Tunafurahia kuwakaribisha wataalamu wa JTC katika ofisi zetu. Ziara hii itawawezesha kuelewa kwa kina namna PBPA inavyoratibu upokeaji wa bidhaa za mafuta na kutumia teknolojia kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa uwazi, usalama na ufanisi,” alisema Bw. Jungulu.

Wataalamu hao pia walipata maelezo kuhusu mchango wa Mfumo wa SCADA katika kuongeza uwazi, usalama na usahihi wa taarifa za kiasi cha mafuta kinachopokelewa nchini.

Akifafanua namna mfumo huo unavyofanya kazi, Mhandisi wa PBPA, Bi. Elvira Muganga, alisema SCADA hukusanya taarifa kutoka kwenye mita za Serikali zilizowekwa katika maeneo ya kupokelea mafuta na kuzilinganisha na taarifa kutoka kwenye mita zilizopo katika maghala ya kuhifadhia mafuta.

“Ulinganishaji huu unasaidia kubaini tofauti zinazoweza kujitokeza wakati wa ushushaji na kuhakikisha kiasi cha mafuta kilichopokelewa kinarekodiwa kwa usahihi,” alisema Bi. Muganga.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Msafara wa JTC, Mhandisi Patrick Mnzava, alisema ziara hiyo imewapa wataalamu hao uelewa zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia katika kusimamia upokeaji na ushushaji wa bidhaa za mafuta.

“Ziara hii imetupa nafasi ya kujifunza kwa vitendo namna PBPA inavyotumia Mfumo wa SCADA kufuatilia upokeaji na ushushaji wa mafuta. Uzoefu tulioupata utatusaidia katika maandalizi na utekelezaji wa mradi wa Bomba Jipya la TAZAMA,” alisema Mhandisi Mnzava.

Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Bomba Jipya la TAZAMA kati ya Tanzania na Zambia, unaolenga kuimarisha usafirishaji na upatikanaji wa bidhaa za mafuta katika nchi hizo.