Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania zaidi ya milioni mbili ambao tayari wamesajiliwa na vitambulisho vyao vya taifa viko tayari, kwenda kuvichukua badala ya kuviacha katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mwigulu alisema hayo leo Septemba 16, 2026 wakati akizungumza katika maadhimisho ya kwanza ya kitaifa ya Siku ya Utambulisho Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho Septemba 16, ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuhamasisha upatikanaji wa utambulisho wa kisheria kwa wote.

Alisema kuwa Serikali imeingia gharama kubwa katika zoezi la usajili na utengenezaji wa vitambulisho hivyo idadi kuna haja ya NIDA kuhakikisha mfumo wa utoaji na ufuatiliaji unaboreshwa.
“Watanzania ambao wameshajisajili na vitambulisho viko tayari waende wachukue,baadhi ya wananchi huacha vitambulisho vyao kwa muda mrefu na kuanza kuvitafuta wanapohitaji huduma ya haraka, hali inayoweza kusababisha usumbufu na kuchelewa kupata huduma,”alisema Dk.Mwigulu.

Dk.Mwigulu pia aliiagiza NIDA kuendelea kuboresha mfumo wa kuwafuatilia na kuwakumbusha wananchi ambao vitambulisho vyao vimekamilika ili waende kuvichukua kwa wakati.
Aidha, aliitaka NIDA kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii, ajira na shughuli za kiuchumi zinaunganishwa na mfumo wa utambulisho wa taifa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uhakiki wa taarifa za wananchi, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza matumizi mabaya ya vitambulisho pamoja na udanganyifu.

Katika hatua nyingine, Dk.Mwigulu alisema Serikali inaendelea na maboresho ya mfumo wa utambulisho wa taifa, ikiwamo kuanza kwa utaratibu wa kuwatambua watoto mapema ili wawe na utambulisho wa kisheria tangu wanapozaliwa.
Alisema utambulisho wa kisheria si suala la kuwa na nyaraka pekee, bali ni msingi unaomwezesha mtu kutambulika kwa usahihi, kupata huduma na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Serikali itaendelea kuunga mkono maboresho yanayofanywa na NIDA, huku akiwataka wananchi ambao hawajasajiliwa kwenda katika ofisi husika kwa ajili ya usajili,”alisema Dk.Mwigulu.

Akizungumzia kuhusu uboreshaji mifumo ya NIDA, Dk.Mwigulu alisema serikali imeeleza kuwa imechukua hatua mbalimbali za kuboresha mfumo wa NIDA, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vitambulisho vyenye teknolojia ya kisasa na viwango vya juu vya usalama.
Alisema katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitenga zaidi ya Shilingi Bilioni 42.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya NIDA, ikiwemo ujenzi wa ofisi 31 za usajili pamoja na kituo kikuu cha huduma za TEHAMA.
Alisema maadhimisho hayo, jumla ya wananchi 27,520,835 wameshasajiliwa, huku watu 23,515,667 wakiwa tayari wamepatiwa namba zao za utambulisho.

Aidha, jumla ya vitambulisho 21,526,635 vimeshazalishwa, lakini zaidi ya vitambulisho 2,027,103 bado vipo katika ofisi za NIDA za wilaya kwa kuwa havijachukuliwa na wananchi.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika NIDA kwa kuboresha miundombinu na teknolojia inayotumika katika usajili na utengenezaji wa vitambulisho.
Alisema uwekezaji huo umehusisha pia utoaji wa magari zaidi ya 20 pamoja na kuboresha mitambo ya kiteknolojia inayotumika kutengeneza vitambulisho vyenye ulinzi wa hali ya juu.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alisema Mamlaka hiyo ipo katika mchakato wa kuboresha Kitambulisho cha Taifa kutoka kuwa na vipengele vinne hadi kufikia vipengele tisa.
Alisema kitambulisho hicho kinatarajiwa kuwa na taarifa mbalimbali muhimu za kijamii, ikiwemo taarifa za cheti cha kuzaliwa, bima ya afya, namba ya mlipa kodi (TIN), leseni ya udereva pamoja na kundi la damu la mwananchi.

“Maboresho hayo yanalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza ulazima wa wananchi kubeba nyaraka au kadi nyingi kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali,”alisema Kaji.
Kaji alisema Serikali, kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), imeanza maandalizi ya mradi wa majaribio wa kusajili watoto mara tu wanapozaliwa.
Alisema mradi huo wa majaribio unahusisha wilaya tatu ambazo ni Kinondoni, Unguja Kusini na Ruangwa, ukiwa na lengo la kuhakikisha watoto wanapata utambulisho wa kisheria mapema.

Aidha, Serikali inaendelea na mipango ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na namba ya utambulisho inayoweza kutumika katika hatua mbalimbali za maisha yake.
Akizungumzia Jamii Namba, alisema ni ileile Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) na kwamba huduma mbalimbali za kijamii zitaweza kutolewa kwa kutumia namba hiyo ya msingi, hatua inayolenga kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali na kurahisisha huduma kwa wananchi.


