Na Mwandiahi Wetu,Morogoro
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha na kuhakikisha uendelevu wa huduma za msaada wa kisheria nchini, ili wananchi wapate haki na huduma za kisheria kwa wakati, kwa ufanisi na bila vikwazo visivyo vya lazima.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Lucy Diganyeck, wakati akifungua Kikao Kazi cha Wasajili Wasaidizi wa Mikoa na Wanasheria wa Mikoa kuhusu uendelevu na uimarishaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini, kilichofanyika tarehe 16 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Morogoro.

Bi. Diganyeck amewapongeza Wasajili Wasaidizi wa Mikoa, watoa huduma za msaada wa kisheria na wadau kwa juhudi zao za kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma za kisheria kwa wakati na kwa ufanisi.
“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha huduma hizo, ikiwemo kupitia Madawati ya Msaada wa Kisheria yaliyopo katika Halmashauri, ambayo hupokea changamoto za kisheria za wananchi na kuwawezesha kupata ushauri na huduma stahiki.

Aliendelea kusema “Madawati hayo yanatoa elimu na ushauri wa kisheria, kuwaelekeza wananchi kwenye taasisi husika, kusaidia usuluhishi wa migogoro pamoja na kutunza taarifa na takwimu za huduma zinazotolewa.”Alisema Bi. Diganyeck.
Amesisitiza kuwa Madawati ya Msaada wa Kisheria hayapaswi kuonekana kama sehemu ya kupokea malalamiko pekee, bali ni nyenzo muhimu katika kuzuia migogoro kabla haijawa mashauri, kutoa elimu ya sheria na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.

Amesema Serikali inatambua kuwa upatikanaji wa haki ni haki ya msingi kwa kila mwananchi, huku wananchi wenye kipato cha chini na makundi maalum, wakiwemo wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na wazee, wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata huduma za kisheria.
Uimarishaji wa huduma za msaada wa kisheria ni muhimu katika kuzuia migogoro, kutoa fursa za usuluhishi, kupunguza mlundikano wa mashauri katika vyombo vya utoaji haki na kutimiza azma ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga mfumo wa haki unaofikika, unaozingatia mahitaji ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.



