📌Miundombinu mipya kuongeza uzalishaji, ubora wa chumvi na kipato cha wanawake
📌Mashine 50 za mkaa mbadala kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia
Na Mwandishi Wetu, Singida
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umejenga miundombinu ya kisasa ya uzalishaji wa chumvi kwa wanawake wa Kijiji cha Nsunsu, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, hatua inayotarajiwa kuongeza tija, kuboresha ubora wa chumvi na kuongeza kipato.
Miundombinu hiyo inatarajiwa kuleta mabadiliko katika uzalishaji ambao kwa muda mrefu umekuwa ukifanyika kwa kutumia mbinu za jadi, kupunguza muda wa uzalishaji na kuongeza kiwango cha chumvi inayozalishwa.

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, amesema Wakala unaendelea kuwekeza katika miradi inayotumia nishati ili kuchochea shughuli za uzalishaji, kuongeza kipato na kuimarisha uchumi wa wananchi wa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Katika hatua nyingine, Mha. Saidy amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali kupitia REA imepanga kuwekeza katika mashine 50 za kuzalisha mkaa mbadala katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa kawaida, hususan kwa wanawake.

Aidha, wanawake wazalishaji wa chumvi Nsunsu wameishukuru Serikali kupitia REA kwa uwekezaji huo, wakieleza kuwa miundombinu hiyo inatarajiwa kuwawezesha kuzalisha zaidi, kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza kipato cha familia zao.
Uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za REA za kuhakikisha nishati inakuwa kichocheo cha uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi vijijini, kwa kuwawezesha wananchi kuongeza tija, kipato na kuboresha maisha yao.


