Mahe, Shelisheli – Juni 28, 2024:
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imeshika nafasi ya pili miongoni mwa Taasisi za Fedha za Maendeleo (DFI) kati ya wanachama kumi na tatu (13) wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). TADB ilishiriki katika tathmini ya Mwongozo wa Viwango vya Kimaadili na Mfumo wa Upimaji (Prudential Standard Guidelines and Rating System – PSGRS) kwa ajili ya Benki na Taasisi za Fedha za Maendeleo barani Afrika mwaka 2022. Ushindi huu ni kwa kutambua mchango wa TADB katika utawala bora, viwango vya kimaadili vya kifedha na ubora wa kiutendaji miongoni mwa Taasisi za Kifedha za Maendeleo za Afrika.
Ushindi huo ulitangazwa wakati wa mkutano wa kamati ndogo ya SADC-DFI uliofanyika Juni 28, 2024, katika Hoteli ya Savoy Seychelles huko Mahe, Shelisheli. Mkutano huu ulihitimisha Mapitio na Upimaji wa 13 wa Taasisi za Fedha za Maendeleo za Afrika, ukijumuisha tathmini ya kina ya taasisi thelathini na nne (34) barani Afrika, kumi na tatu (13) kati ya hizo zikiwa ni wanachama wa mtandao wa DFI za SADC.
Mchakato wa tathmini kwa kutumia Mwongozo wa Viwango vya Kimaadili na Mfumo wa Upimaji (PSGRS) ulijumuisha kujitathmini kwa umakini na kisha kuthibitishwa na wakaguzi wa nje kabla ya kuwasilishwa kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Taasisi za Fedha za Maendeleo ya Afrika (AADFI) kwa tathmini huru, na hatimaye kupata alama kwa mujibu wa viwango vya PSGRS.
TADB ilipata alama 91% na kushika nafasi ya pili baada ya “Gapi-Sociedade de Investimentos” kutoka Msumbiji, iliyopata alama 92% miongoni mwa DFI za SADC. Washiriki wengine muhimu walijumuisha Benki ya Maendeleo ya Angola, Benki ya Akiba ya Botswana, Benki ya Maendeleo ya Namibia, Benki ya Maendeleo ya Shelisheli, Benki ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Shirika la Maendeleo ya Viwanda “South Africa”, Shirika la Fedha za Maendeleo la Eswatini, Mfuko wa Maendeleo ya Usafirishaji (Malawi), Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Zimbabwe, Shirika la Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati (Zimbabwe), na Benki ya Maendeleo ya TIB (Tanzania).
Tathimini ya PSGRS kwa ajili ya Benki na Taasisi za Fedha za Maendeleo iliandaliwa na Jumuiya ya Taasisi za Fedha za Maendeleo ya Afrika (AADFI) kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Tathmini ya PSGRS sio tu inatathmini nguvu za taasisi na maeneo yanayohitaji kuboreshwa bali pia inatumika kama kipimo muhimu kwa viwango vya kimataifa vya mikopo na kuboresha upatikanaji wa masoko ya mitaji.
Akionyesha furaha yake kuhusu nafasi ya TADB, Mkurugenzi Mtendaji Bw. Frank Nyabundege, alibainisha kuwa utawala bora, usimamizi wa kifedha wa kimkakati, pamoja na uwezeshwaji wa kifedha kutoka serikalini unaolenga kuongeza utoaji wa mikopo katika sekta ya kilimo vilikuwa ni nguzo muhimu iliyosaidia mafanikio ya TADB. Alisema, “Tunashukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. TADB inaendelea kujidhatiti katika kutimiza dhamira zake kuu, ikilenga kuchagiza maendeleo ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara pamoja na kuchangia utoshelevu na usalama wa chakula nchini Tanzania”