NPCC YATOA ELIMU YA KUJIKINGA NA SUMU YA NYOKA KWA WANAFUNZI

Na Mwandishi Wetu,Pwani
Katika kuadhimisha Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), imetoa elimu kuhusu sumu ya nyoka na namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na kung’atwa na nyoka kwa wanafunzi na walimu wa shule za msingi zilizopo Kibaha mkoani Pwani.


Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Yohana Goshashy amesema utoaji wa elimu kwa wanafunzi ni sehemu ya jitihada za Mamlaka kuongeza uelewa wa jamii kuhusu sumu na namna ya kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matukio ya sumu, ikiwemo kung’atwa na nyoka.


“Dhumuni la kutoa elimu hii kwa wanafunzi ni kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu nyoka wenye sumu, namna ya kujikinga na kung’atwa pamoja na hatua sahihi za kuchukua endapo tukio hilo litatokea. Tunataka wanafunzi wajue kwamba kung’atwa na nyoka ni tukio linalohitaji hatua za haraka na sahihi za kitabibu, hivyo ni muhimu kumfikisha mgonjwa kwenye kituo cha afya mapema,” alisema Goshashy.


Amesema wanafunzi ni kundi muhimu katika jamii kwa kuwa elimu wanayoipata shuleni inaweza kuwasaidia kujilinda wao wenyewe, kuwasaidia wenzao na pia kufikisha ujumbe huo kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Aidha, ameongeza kuwa baadhi ya imani na taratibu zisizo sahihi zinazofanywa na jamii baada ya mtu kung’atwa na nyoka zinaweza kuongeza madhara kwa mgonjwa, hivyo ni muhimu jamii kupata elimu sahihi kutoka kwa wataalamu.

“Tunasisitiza jamii kuacha kutumia njia zisizo salama katika kumhudumia mtu aliyeng’atwa na nyoka. Mtu aliyeng’atwa anapaswa kupata huduma ya kitabibu haraka iwezekanavyo. Elimu hii tunayoitoa shuleni inalenga pia kuwafanya wanafunzi wawe mabalozi wa ujumbe huu katika familia zao na kwenye jamii,” alisisitiza Goshashy.


Kwa upande wake, Mwalimu anayesimamia masuala ya Afya katika Shule ya Msingi Kanesa iliyopo Kibaha mkoani Pwani, Fatuma Nkya ameeleza kuwa elimu hiyo imekuwa na faida kubwa kwa wanafunzi na walimu kwa sababu imewaongezea uelewa kuhusu namna ya kutambua hatari zinazohusiana na nyoka pamoja na hatua za kuchukua pale tukio la kung’atwa linapotokea.

Amesema kabla ya elimu hiyo, baadhi ya wanafunzi na hata watu katika jamii wanaweza kuwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu namna ya kumsaidia mtu aliyeng’atwa na nyoka, jambo ambalo linaweza kuchelewesha upatikanaji wa matibabu.


“Elimu hii imekuwa muhimu sana kwetu kwa sababu imewasaidia wanafunzi na walimu kufahamu mambo ambayo awali hatukuwa na uelewa wa kutosha. Sasa tunajua umuhimu wa kuchukua hatua kwa haraka na kumpeleka mhanga kwenye kituo cha afya badala ya kutumia njia ambazo hazijathibitishwa kitaalamu,” alisema Nkya.


Alisema wanaishukuru Mamlaka kwa kufikishia elimu hiyo. Na wanawaona wanafunzi kama sehemu muhimu ya kusambaza elimu hii kwa sababu wanapofundishwa jambo muhimu, wanaweza kwenda kuwaeleza wazazi, ndugu na marafiki. Hivyo, elimu hiyo haibaki shuleni pekee, bali inakwenda hadi kwenye jamii.


Naye mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo kutoka Shule ya Msingi Kanesa, Samir Kadili ameipongeza Mamlaka kwa kuwafikishia elimu hiyo, akisema imewasaidia kufahamu namna ya kujikinga na nyoka na nini cha kufanya endapo mtu atang’atwa.


“Tunawashukuru Mamlaka kwa kutupatia elimu hii kwa sababu tumefahamu mambo ambayo hatukuyajua. Tumejifunza kuwa tunapaswa kuwa makini tunapokuwa maeneo ambayo kuna uwezekano wa kuwepo kwa nyoka na pia tumeelewa umuhimu wa kumpeleka haraka hospitalini mtu aliyeng’atwa,” alisema Kadili.


Elimu hiyo ni sehemu ya shughuli za Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa, ambayo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kuzuia matukio ya kung’atwa na nyoka, kutambua hatari zinazohusiana na sumu ya nyoka na kuchukua hatua sahihi pindi tukio linapotokea.