COPRA YAWEKA MIKAKATI KUMI YAKUONGEZA UZALISHAJI NGANO

Na  Aziza Masoud, Dar es Salaam 

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), imeandaa mkakati wa miaka 10 wa kuongeza uzalishaji wa ngano.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha wadau wa zao la ngano,Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola  zao hilo pamoja na kuwa ni miongoni mwa  mazao muhimu limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kukwamisha ukuaji wa zao hilo.

Alisema kuwa Sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo wa ngano ambapo inakadiriwa ni wastani wa Tani 100,000 zinazozalishwa nchini ikilinganishwa na Tani takribani milioni moja ambayo ni matumizi ya ndani ya nchi.

“Sekta ya ngano ina mchango mkubwa katika uchumi wa Nchi ambapo tunajua sekta ya kilimo huchangia asilimia 26 ya Pato la Taifa na inaendelea kuwa mwajiri nkuu nchini kwani asilimia 65 ya Watanzania wameajiliwa kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo.

“Tunajua tumebarikiwa sana, tuna ardhi, maji, watu, uwezo lakini kama nchi bado tunaingiza ngano ambapo takribani asilimia 90 tunayokula inatoka nje ya nchi. Hii ndo sababu ya kukutana hapa… Lakini katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali imeona kuna umuhimu wa kuandaa mkakati wa kuendeleza zao la ngano nchini ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 mpaka mwaka 2035,” amesema.

Amefafanua kuwa, mkakati huo umejikita katika kuongeza uzalishaji wa ngano kutika tani 100,000 ili zifike tani  milioni 1.5 ifikapo mwaka 2035.

“Ili hayo tuweze kufanikisha tumewasikia wataalam wetu wametuambia kuna juhudi nyingi ambazo zimefanyika ikiwemo kuongeza mbegu bora za ngano zifikie tani 64,266 ili kuweza kukamilisha huu mpango tuliouweka.

“Lakini vilevile upatikanaji wa mbolea ni muhimu sana kwani mpaka Januari 31,2025 katika mikoa ambayo inazalisha ngano zimepatikana laki 247,000 na usambazaji wa mbolea hizo bado unaendelea. Kwahiyo tunaona jinsi ambavyo serikali imeweza kuwekeza kwenye pembejeo na kuwa na mikakati ya makusudi kuhakikisha kweli tunaenda kuongeza uzalishaji,” amesema.

Ameongeza kuwa, Serikali inaenda kukamilisha upimaji wa afya ya udongo nchi nzima na kuandaa ramani yake ya udongo pia inajenga maghala na kukarabati 15 ambayo yapo kwenye maeneo ya uzalishaji wa ngano pamoja na kujenga vituo vitano vya kutoa huduma za zana za kilimo katika maeneo yanayozalisha ngano nchini na kuendeleza kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yenye ukubwa wa hekta 100,000 ifikapo 2035 ambapo yatakuwa yanazalisha zao la ngano.

Aidha amesema bado kuna changamoto kubwa kwenye kilimo cha mikataba kati ya wakulima wanunuzi na wasindikaji kwasababu hawana kanuni ya kusimamia mikataba hiyo.

Mkulima wa zao la ngano kutoka Kilimanjaro, Isaya Mollel amesema wanakabiliwa na changamoto ya masoko.

“Huku kwetu mnunuzi wa ngano ni mmoja tu ambapo kuna wakati anazidiwa hali inayopelekea kushindwa kutulipa kwa wakati,” amesema Mollel.

Katika kikao hicho ambacho kimejadili mambo muhimu yanayohusu maendeleo ya zao la ngano ikiwa ni pamoja na mikakati ya kuimarisha uzalishaji wa zao hilo na ushirikiano kati ya serikali na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *