Na Mwandishi Wetu,Morogoro
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, amewapongeza watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao katika kusimamia kwa umakini mitambo mbalimbali ya umeme nchini
Dkt. Kazungu ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa mitambo ya umeme Mtera Januari 5, 2025 huku akisisitiza zaidi umuhimu wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika ili kuepusha malalamiko yanayotokana na changamoto za umeme.
Dkt. Kazungu amewataka watumishi wa TANESCO kuendelea na juhudi zao za usimamizi wa mitambo hiyo ili kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inapatikana kwa wingi na kwa uhakika. “Ni muhimu wananchi wapate umeme ili waweze kufaidika na shughuli mbalimbali za maendeleo kama viwanda, kilimo, na biashara, ambazo ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.”
Aidha, amemtaka mkandarasi anayekarabati chumba cha kuongozea mitambo kituo cha Mtera kuhakikisha kuwa anaweka vifaa vya kisasa ili kuwezesha kazi kufanyika kwa ufanisi
Akizungumza, Meneja wa Kituo cha Mtera, Mhandisi Edmund Seif, amesema TANESCO inaendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha usalama wa vyanzo vya maji vya bwawa la Mtera, ambalo ni muhimu kwa uzalishaji wa umeme nchini, Kwa kushirikiana na vyombo vinavyosimamia rasilimali maji.
Aidha ameeleza kuwa kwa kuwepo na utunzaji bora wa vyanzo hivyo kutadumisha ufanisi wa mitambo ili kuepuka changamoto za ukosefu wa maji ambayo inaweza kuathiri uzalishaji wa umeme na kusababisha athari kwa jamii inayotegemea nishati hiyo.
Amesema TANESCO imejidhatiti pia kufanya matengenezo ya mara kwa mara na kwa wakati ili kuongeza uimara wa mitambo na kuhakikisha kuwa wanatoa huduma za umeme kwa usahihi na kwa wakati.