Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WATOTO 400 wenye uhitaji kutika vituo tofauti vya kulelea watoto wamekabidhiwa vifaa mbalimbali vya shule vikiwemo mabegi,sare za shule,soksi na viatu.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa na Taasisi ya Lalji Foundation mbele ya Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaluumu Mwanaidi Ally Khamis ambapo ameipongeza taasisi kwakuwasaidia watoto hao ambapo wengi wao hawana wazazi.
Naibu Waziri Mwanaidi pamoja na kuishukuru taasisi hiyo pia aliwasihi watoto wote nchini wazingatie masomo shuleni ili kufikia malengo yao.
“Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassani ameweza kutoa fursa za kusoma shuleni bila malipo,wito wangu kwa wazazi wote nchini kuhakikisha kuwa mtoto kama umri wake umefika wa kuanza shule apelekwe shuleni kwani elimu inatolewa bure nchini kote watoto pia mnapaswa kusoma kwa bidii,”amesema Naibu Waziri Khamis.
Amesema wizara inatoa huduma mbalimbali ili kuweza kuimarisha huduma za jamii nchini zikiwemo malezi ya watoto, Sheria na shughuli zote ambazo zinashughulikia makuzi na maendeleo katika wizara yetu.
“Sisi kama wizara tunahakikisha kuwa Tunasimamia na kuratibu mambo kadhaa yakiwemo watoto yatima na watoto waliozaliwa nje ya ndoa,’amesema.
Awali Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Imtiaz Lalji amesema kuwa kama taasisi wanatoa huduma za msingi kwa watu wenye uhitaji kama hao watoto ambao tumeweza kuwapita vifaa vya shule hivyo tunatarajia watoto hawa wanaenda kutumiza malengo yao shuleni kwani vifaa muhimu vya shule wameshapata kwa wakati.
Naye Katibu wa Lalji foundational Fatma Lalji amesema taasisi hiyo mbali na kuwasaidia watu wenye mahitaji pia imeweza kukabidhi vifaa mbalimbali nchini ikiwemo hosptali ya CCBRT kwa kuchangia miguu bandia kwa wenye uhitaji.
Vilevile tunatoa vifaa kwa mwaka mara mbili mwanzo wa mwaka na mwishoni mwa mwaka katika sehemu zenye uhitaji lengo ni kuweza kupeleka huduma kwa jamii husika ikiwemo watoto walioko kwenye vituo maalumu.