Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WANAWAKE wanaobandika kope bandia wametakiwa kuchukua tahadhali kwakuwa wapo katika hatari ya kupata magojwa mbalimbali ya macho ikiwemo trakoma (vikope) na tatizo la uoni hafifu.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam Leo Januari 21, mwaka 2025 na Afisa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magojwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele (NTDCP) kutoka Wizara ya Afya,Dk.Lilian Lyatura wakati wa semina kwa waandishi wa habari kuhusu Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele iliyoandaliwa na wizara hiyo kuelekea siku maalum ya maazimisho ya siku hiyo yatakayofanyika Januari 30.

Amesema magonjwa ya trakoma na huoni hafifu yanasababishwa na kovu linalotokana na msuguano katika kioo cha jicho jambo ambalo linaweza kusababishwa pia ubandikaji wa kope.
“Kope za bandia jinsia zinavyowekwa ni hatari sana,zina uwezo mkubwa wakusugua jicho na ikisugua kioo cha jicho inaweza kusababisha trakoma na huoni hafifu,”amesema Dk.Lilian.

Amesema msuguano ya kwenye kioo cha jicho ikifanyika hata kwa kope za kawaida pia zinaleta changamoto ya macho.
Akizungumzia ugonjwa wa trakoma alisema ni ugonjwa unaoshambulia macho na kusababisha kope kupinda na kugusa kioo cha jicho ambayo husababisha makovu juu ya kioo cha jicho.

“Ugonjwa huu huenezwa na nzi aliyebeba vimelea vya ugonjwa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwa mtu asiye na maambukizi,”amesema Dk.Lilian.
Kuhusu hali ya maambukizi Dk.Lilian alisema halmashauri zilizokuwa na maambukizi ya juu zaidi ya asilimia tano ya ugonjwa wa trakoma zilikuwa 69.

“Baada ya kutoa kingatiba aina ya zithromax zimepungua hadi kufikia halmashauri tisa ambazo ni Longido,Ngorongoro,Monduli,Kiteto,Simanjiro,Kalambo,Mpwapwa,Kongwa na Chamwino,”amesema Dk.Lilian.
Katika semina hiyo wana habari wameelimisha kuhusu magojwa yasiyoambukizwa yakiwemo trakoma,usubi,matende na ngiri maji,kichocho na minyoo ya tumbo.
