BENKI YA EQUITY YAFUTURISHA WATEJA,WADAU MJI MKONGWE ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu,Zanzibar

BENKI ya Equity siku ya jana iliandaa tukio la kipekee la Iftar, likiwa na lengo la kuleta pamoja wadau muhimu, wakiwemo viongozi, wateja, na wadau mbalimbali, ili kusherehekea kwa pamoja katika mwezi huu wa Ramadhani. Iftar hiyo ilifanyika katika hotel ya Madinat Al Bahr.

Katika hotuba yake,Mkuu wa Kitengo cha Malipo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Equity Tanzania Haidari Chasama alikaribisha wageni na kutoa shukrani za dhati kwa wote waliohudhuria tukio hilo kwa niaba ya Menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya Equity .

” Shukrani za kipekee zilielekezwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mheshimiwa Omary S. Shaaban, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo,ni furaha kubwa kuwa na wewe hapa leo, Mheshimiwa Waziri.

“Uongozi wako umejikita katika kukuza sekta ya biashara na viwanda Zanzibar. Juhudi zako ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wetu, na sisi kama benki tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii ya maendeleo,”alisema Chamshama.

Amesema tukio hilo lilikuwa fursa ya kuonyesha shukrani kwa wateja waaminifu wa Benki ya Equity, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya benki.

“Kama benki, tunatambua kwamba hatuwezi kufanikiwa bila ya ushirikiano wenu. Leo(jana) hii, tunasherehekea mafanikio yetu kwa kushirikiana nanyi, na tunaendelea kujitahidi kuboresha huduma zetu kila siku,” ameongeza Chamshama.

Amesema katika kipindi cha Ramadhani mshikamano, kusaidiana, na huruma kwa wengine ni muhimu, Benki ya Equity imejizatiti kutoa huduma bora kwa jamii.

Amesema benki inatambua na inajivunia katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma zetu bora na bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja wake. Na tunaahidi kuendelea kuleta huduma bora zinazoendana na kasi ya tekinolojia.


Kwa kumalizia, Chamshama aliwaomba wadau na wateja wote waendelee kutumia huduma za benki na kuwatakia Ramadhan njema.

“Kwa niaba ya Benki ya Equity, natakieni Ramadhani yenye amani, furaha, na mafanikio. Mfungo wenu uwe wa baraka na mafanikio.”

Tukio lilimalizika kwa dua na Iftar, ambapo wageni walifurahia mshikamano na roho ya kujitolea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *