Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
MGOMBEA wa nafasi ya udiwani Kata ya Saranga kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi John Sanga, amesema ameomba ridhaa ya wananchi ili aweze kushughulikia changamoto zilizopo katika kata hiyo, ikiwemo kumalizia asilimia 15 iliyobaki ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza Oktoba 11, 2025 katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika kwa hadhara, Mhandisi Sanga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada ilizofanya hadi sasa, ambazo zimewezesha kata hiyo kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji.
“Sifahamu changamoto za Saranga kwa kuhadithiwa, nazijua kwa kujionea kwa macho yangu mwenyewe. Ndiyo maana nimeomba kuwa diwani, ili nichukue hatua za kuzitatua kwa vitendo,” alisema.

Mhandisi Sanga ameongeza kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuwa diwani, atahakikisha anatekeleza mahitaji ya wananchi wa Saranga kwa asilimia 100, huku akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinatekeleza Ilani yake kwa vitendo na si maneno matupu.
“CCM haiahidi kwa makaratasi tu, bali inatekeleza kwa ushahidi wa macho. Ushahidi huu unaonekana hapa Saranga,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Sanga aliwaomba wananchi wa Saranga kumpigia kura ya ndiyo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba, Angellah Kairuki, ili waweze kuendeleza mafanikio ya miaka mitano ijayo (2025–2030).
Amesema Rais Samia ameonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi katika kipindi cha miaka minne, na kuwa mfano wa kuigwa kwa uhodari wake wa kusimamia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, kada wa CCM aliyehudhuria mkutano huo, alisema kuwa Oktoba 29, mwaka huu, Kata ya Saranga itaibuka kinara wa kura nyingi katika Jimbo la Kibamba.
“Tumejipanga vya kutosha. Kata ya Saranga hakuna wa kutuzuia. Ushindi wa CCM katika kata hii hauna mbadala,” alisema.
