Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na World Maritime University (WMU) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika elimu ya masuala ya bahari, tafiti na maendeleo ya uwezo wa taasisi. Hafla ya utiaji saini imefanyika Februari 26, 2026 katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza.
Utiaji saini huo umefanywa na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Tumaini Gurumo na Rais wa WMU, Prof. Dk. Maximo Q. Mejia, Jr, mbele ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki, aliyekuwa mwenyeji wa hafla hiyo.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza taaluma na utaalamu wa sekta ya uchumi wa buluu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kairuki amesema Tanzania ina jukumu la kuhudumia si tu uchumi wake, bali pia nchi jirani zisizo na bandari, akisisitiza kuwa nguvu ya bahari ni rasilimali ya taifa na wajibu wa kikanda.

Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji katika miundombinu lazima uendane na uwekezaji kwa watu kupitia ujuzi, tafiti na kuzingatia viwango vya kimataifa.
Makubaliano hayo yamelenda Ushirikiano katika programu za mafunzo ya pamoja kati ya Afrika na Ulaya, maendeleo ya mifumo ya takwimu za elimu ya bahari, tafiti za usalama wa vyombo vya majini ikiwamo jahazi za jadi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi, ubadilishanaji wa kitaaluma, uboreshaji wa mitaala na kuimarisha uwezo wa taasisi.
Pande hizo zimeahidi kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuimarisha sekta ya bahari na uchumi wa buluu nchini.






