Na Mwandishi Wetu,Morogoro
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Saida Mhanga amesema, Serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha ulinzi wa mtoto unaimarika kwa kuwa, Tanzania imara ya kesho inategemea malezo bora ya watoto leo.
Saida alitoa kaulio hiyo jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika na Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika kwa pamoja katika Viwanja vya Shule ya Msingi Igawa, Kata ya Malinyi Mjini.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika utoaji wa elimu bure, afya ya Mama na Mtoto.
“Wilaya ya Malinyi imepokea fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utoaji elimu, zahanati, Vituo vya Afya, Mahakama, Kituo cha Polisi, Miradi ya Maji Chuo cha VETA ili kuandaa kesho ya watoto wetu,” alisema.

Kwenye maadhimisho hayo ambayo awali yalipangwa kufanyika tarehe 16 Juni na Siku ya Familia Duniani tarehe 30 Juni, yalifanyika jana kutokana na muingiliano wa ratiba katika Wilaya ya Malinyi alisema,ulinzi wa mtoto unaanzia kwenye familia.
Kiongzi huyo alisema, Taifa lolote linalotaka kusimama imara, huanzia nyumbani kwa huko ndiko kwenye kiwanda cha kwanza cha kutengeneza raia bora, malighafi kuu ikiwa ni mtoto na mafundi wake wakuu ni wazazi na walezi.
Alisema, mtoto anayekuwa kwa upendo, nidhamu, maadili na elimu ndio nguzo ya familia bora na familia bora ndizo zinazojenga Malinyi na Taifa imara.

“Mtoto anayejengwa kwa tabia bora, anakuwa msingi imara wa Taifa lakini mtoto asiyelelewa vizuri leo, ni changamoto kubwa kwa Taifa baadaye.
“Malezi si kumpa mtoto chakula na nguo tu, ni kusimamia malezi yake katika muda wake wote wa malezi ikiwa ni pamoja na kusimamia elimu yake sambamba na kuhakikisha asijiingize kwenye makundi yasiyofaa,” alisema Saida.
Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, vongozi wa dini, vikosi vya ulinzi na usalama, wazee wa kimila, wazazi na walezi Katibu Tawala huo alisema, familia imara zina mchango mkubwa katika kuhakikisha malezi bora ya mtoto.

Na kwamba, ugomvi katika familia unaathiri kwa kiwango kikubwa malenzi ya watoto.
Alisema, Tanzana inahitaji kuwa na kizazi kitakachoweza kutumika kwa maslahi ya Taifa huku wakitambua thamani ya tunu ya amani na usalama kwa wanaowazunguka.
“Baba na Mama ndio nguzo bora katika familia, sasa hivi tunashuhudia ugomvi wa wazazi unaanzia ndani mpaka Serikali ya Mtaa, hapo mtoto anajifunza nini? Hili sio jambo bora kabisa?
Aliwaomba viongozi wa dini kusaidia malezi kwa watoto na familia huku akiwakumbusha wanafunzi kukataa lifti za bodaboda na magari, kupewa pipi mtaani pia kudanganywa kwa chipsi.

Afisa Maendeleoya Jami katika Halmashau ya Wilaya ya Malinyi, Rehema Kapungu alisema, ushirikiano katika malezi hutoa matokeo yenye manufaa kwa jamii.
“Ukiona mtoto wa mwenzako anafanya yasiyokubalika, usisema huyu hanihusu maana tabia zinaambukizwa, chukua hatua hata kwa kuanzia kwa wazazi wake lakini pia kwenye vyombo husika,” alisema huku akongeza;
“Kwenye familia zetu kama hakuna maelewano, ni vigumu mno watoto kupata malezi bora. Tunapaswa kutatua migogoro yetu ya kifamilia kwa amani na tuvumiliane jamani.”
Rashidi Kiding’o ambaye ni Mwenyekiti wa Kituo Msaada wa Kisheria Malinyi alisema, katika kukabana na matuko ya kikatili, Watoto wanapaswa kuendelea kutoa taarifa kuhusu matukio ya kikatili wanayokutana nayo.
“Ukatitili wa kijinsia unaathiri ndoto za watoto kwa kiwango kikubwa, tunapaswa kuwalinda watoto wetu,” alisema na kuongeza;
“Hata hivyo, wazazi wanapaswa kutoa malezi mazuri kwa watoto wao kwa kuwa, ni wajibu wao kisheria.”
Katika risala iliyosomwa na Juliet Natonga kwa niaba ya wazazi, alieleza kubadili usimamizi na malezo ya mtoto kwa kuwa nao karibu zaidi.
“Tunatubu na tunajipanga upya kuwalea watoto wetu. Tutawalinda na kuchukua hatua stahiki pale inapofaa kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla,” alieleza Natonga.
Shangwe Mlela, Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi Malinyi alisema, watoto wa Malinyi ni hazina na wao kama viongozi, wazazi na walezi wana wajibu wa kuwalinda dhidi ya ukatili, utumikishwaji, vitendo viovu, ndoa za utotoni na utoro shuleni.
Aliwaambia elimu yao ndio urithi ambao hakuna mtu yeyote wa kuweza kuwanyang’anya, hivyo wasome kwa bidii.
Maadhimisho hayo yalipambwa kwa zawadi katika shule zote, burudani mbalimbali za nyimbo, ngonjera, maigizo, kucheza dansi, mashairi, ngoma za asili huku Kauli Mbiu ikiwa ni ” Mtoto ni Malezi Msingi wa Familia Bora kwa Taifa imara”


