PROFESA MBARAWA:ENEO LA KUHIFADHIA KONTENA KURASINI KUANZA KAZI NOVEMBA 2026

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema eneo jipya la kuhifadhia makontena linaloandaliwa kwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam (Port Extension) linatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Novemba 2026, hatua inayolenga kupunguza msongamano bandarini na kurahisisha upatikanaji wa mizigo kwa wafanyabiashara.

Profesa Mbarawa alisema hayo jana  wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa eneo hilo, ambapo ameeleza kuwa utekelezaji umefikia asilimia 98 kutoka asilimia 90 wakati wa ziara yake ya awali.

 Alisisitiza kwa sasa umuhimu  si kuongeza asilimia ya ujenzi, bali kuhakikisha eneo hilo linaanza kufanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi na watumiaji wa bandari.

“Katika hatua ya kwanza eneo hilo litahudumia makontena ya mizigo inayoingia nchini, ambapo baada ya kushushwa katika Bandari ya Dar es Salaam, mizigo hiyo itahamishwa hadi eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi na taratibu za forodha. Ili kuhakikisha usalama na udhibiti wa mizigo, Serikali imepanga kupeleka mobile scanner, huku barabara inayounganisha eneo hilo na bandari ikitambuliwa kama customs-bound road kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo chini ya usimamizi wa mamlaka za forodha,”alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amesema awamu ya kwanza ya Port Extension hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani makontena 150,000, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuongeza uwezo hadi makontena 700,000.

 Ameeleza kuwa TPA, na Mamlaka ya  Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine za Serikali zitatoa huduma katika eneo hilo, hatua ambayo itasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa utoaji wa mizigo kwa wafanyabiashara na wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Galcus Abed, alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) itatekeleza maelekezo ya Serikali kuhakikisha Kurasi Logistics Park inatumika ipasavyo katika kupunguza msongamano wa malori na mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam. Amesema kuongezeka kwa shughuli za bandari pamoja na kukua kwa jiji kumeongeza shinikizo kwenye miundombinu ya barabara na usafirishaji wa mizigo.

Abed alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja, kiwango cha mizigo katika bandari hiyo kimeongezeka kwa takribani tani milioni sita, hali iliyoongeza mahitaji ya maeneo ya nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhi malori na mizigo. 

Alisema Kurasi Logistics Park imeandaliwa kuwa sehemu muhimu ya kupokea na kuhifadhi malori pamoja na mizigo kabla ya kuondolewa bandarini, hivyo kusaidia kupunguza msongamano unaotokana na shughuli za kibandari.

“Naishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miundombinu hii  tunaahidi kuwa TPA itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha Kurasi Logistics Park inatumika kwa ufanisi,”alisema.

Alisema matumizi bora ya eneo hilo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na ongezeko la mizigo, msongamano wa malori na mahitaji makubwa ya huduma za usafirishaji katika Bandari ya Dar es Salaam.