ZAIDI YA 95% YA WALIOHUSIKA NA UJENZI BWAWA LA MWALIMU NYERERE NI WATANZANIA- TWANGE

Na Mwandishi Wetu,Rufiji

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Jacob Twange, amesema ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere umewezesha Watanzania kupata ujuzi na uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, jambo litakalowaongezea uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Twange amesema hayo leo Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere mkoani Pwani.

Amesema zaidi ya asilimia 95 ya waliofanya kazi katika ujenzi wa mradi huo walikuwa Watanzania, hivyo uzoefu walioupata utawasaidia kupata ushindani katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Twange pia amesema mhandisi mshauri wa mradi huo alikuwa Mtanzania, akieleza kuwa ushiriki wake umejenga uwezo zaidi kwa wataalamu wa ndani na kuthibitisha kuwa Watanzania wana uwezo wa kusimamia miradi mikubwa na kuikamilisha kwa wakati.

“Mhandisi mshauri pia alikuwa Mtanzania, tunaamini naye amejenga uwezo kwa kushiriki katika mradi huu na imeonesha kuwa watanzania tunao uwezo wa kusimamia miradi mikubwa na ikamalizika kwa wakati na yeye mwenyewe pia amejenga uwezo kwamba anaweza kushindana popote akiomba kazi za miradi ya ujenzi.”

“Kituo hiki pia tunaamini kinaenda kuwa muhimili wa usalama wa Taifa letu, kwahiyo tunakuahidi Mhe. Rais kuwa tutaongeza na kuboresha mifumo yetu ya udhibiti, matengezo ili kuepuka dosari kwenye mitambo yetu lakini pia tutaendesha kushirikiana na wenzetu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha panakuwa na ulinzi madhubuti ili kuepusha hatari mbalimbali.”

Aidha, amesema uendelevu wa uzalishaji umeme katika bwawa hilo unategemea upatikanaji wa maji, hivyo TANESCO itaendelea kushirikiana na wadau wa mazingira katika kulinda vyanzo vya maji vinavyolisha bwawa hilo.