TANZANIA SASA INA ZIADA YA MEGAWATI 2,375 ZA UMEME, KUANZA KUUZA NJE- NDEJEMBI

Na Mwandishi Wetu,Rufiji

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema uzinduzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ni matokeo ya juhudi kubwa za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuongeza uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme.

Ndejembi amesema hayo leo Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo mkoani Pwani mbele ya Rais Samia, akieleza kuwa kituo hicho kina jumla ya mitambo tisa, ambapo kila mtambo una uwezo wa kuzalisha megawati 236, na hivyo kufikisha jumla ya megawati 2,115.

Amesema ongezeko hilo la uzalishaji limeongeza uwezo wa Tanzania kukidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi na uwekezaji, huku likiiweka nchi katika nafasi muhimu ya kuunganisha soko kubwa la nishati ya umeme barani Afrika kupitia ushiriki wake katika mipango na miundombinu ya kuunganisha mitandao ya umeme kikanda.

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme kwa sasa umefikia megawati 4,646, wakati mahitaji ya juu ya Gridi ya Taifa ya megawati 2,271, hali inayosababisha kuwepo kwa ziada ya megawati 2,375.

Amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia, imeelekeza nchi kuanza kutumia fursa hiyo kufanya biashara ya umeme na mataifa jirani, ambapo tayari Tanzania imeingia makubaliano na Zambia kwa ajili ya kuiuzia umeme.

Aidha, Ndejembi amesema Tanzania ina makubaliano na Serikali ya Kenya ya kuuziana umeme kulingana na mahitaji ya kila nchi, huku Serikali ikiendelea na mazungumzo na nchi nyingine jirani ili kuwezesha biashara ya umeme pale inapohitajika.